• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
TAHARIRI: Waliokabili magaidi fahari kwa Kenya

TAHARIRI: Waliokabili magaidi fahari kwa Kenya

NA MHARIRI

Shambulio la kigaidi lililotekelezwa juzi jijini Nairobi na magaidi wenye makao yao nchini Somalia, Al-Shabaab, ni thibitisho kwetu kama nchi kwamba, bado kuna haja ya kuchukua kila tahadhari na kumakinika nyakati zote.

Kama tulivyowahi kutaja kwenye safu hizi, magaidi hawana chembe ya utu na hivyo hawatachelea kumwaga damu ya binadamu wenzao wasio na hatia.

Kwa hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kila hatua inachukuliwa kujiepusha na hali ambayo itarahisisha visa vyovyote vya uvamizi kama tukio la hivi majuzi.

Magaidi hao wamejaribu kila mbinu kuzua mgawanyiko wa kidini na kikabila nchini. Lakini kila wanapotekeleza vitendo hivyo kwa lengo la kuzua uhasama na mgawanyiko wa kijamii, udugu baina ya Wakenya unaimarika hata zaidi.

Kwa sasa, tunaungana na Wakenya wengine kuwalimbizia sifa na shukrani tele maafisa wetu wa usalama kwa ujasiri wao mkubwa katika kudhibiti hali hii ambayo ingegeuka kuwa maafa mabaya zaidi.

Kinyume na hapo awali ambapo walinda usalama walijikokota kufika katika eneo la mkasa kama huo, hali ilikuwa tofauti kwenye shambulio la juzi.

Vikosi mbalimbali vya usalama vilionyesha ustadi wao baada ya kulemaza magaidi hao kwa muda mfupi mno, licha ya kuwachukua mateka baadhi ya wageni kwenye hoteli ya Dusit kama ngao yao.

Kutokana na hatua hiyo, umwagikaji mkubwa wa damu uliepushwa huku magaidi wote waliohusika kwenye shambulio hilo wakiangamizwa.

Kwa mara nyingine, Wakenya wa kawaida walidhihirishia ulimwengu mzima kwamba, licha ya changamoto za hapa na pale za kisiasa na kiuchumi, bado tu watu wa jamii moja pana ijulikanayo kama Kenya.

Wengi walimiminika katika hospitali mbalimbali kutoka Nairobi hadi Mombasa kutoa damu. Baadhi wakaandaa chakula cha kuwalisha maafisa wetu wa usalama huku wengine wakihatarisha maisha yao kuwanusuru Wakenya wenzao waliozuiliwa katika jengo hilo kuu.

Kutokana na weledi mkubwa waliodhihirisha walinda usalama wetu wakati wa shambulio la juzi, kuna haja ya kupanua vikosi maalumu kama kile ambacho kimegeuka kuwa kipenzi cha Wakenya-Recce Squad- ili viweze kukabiliana na magaidi kama hao kwa urahisi.

Kwa mara nyingine, heko kwa maafisa wetu wa usalama!

You can share this post!

Magaidi hawana dini wala kabila – SUPKEM

AKILIJIBU: Naomba kujua manufaa ya mkojo wa sungura

adminleo