• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Spurs sasa yamtaka Origi kuimarisha mashambulizi

Spurs sasa yamtaka Origi kuimarisha mashambulizi

Na GEOFFREY ANENE

TOTTENHAM Hotspur sasa inatafuta huduma za Divock Origi kutatua idara yake ya mashambulizi baada ya mchana-nyavu matata Harry Kane kuthibitishwa atakuwa nje hadi mwezi Machi akiuguza jeraha la kifundo.

Spurs, ambayo imeajiri Mkenya Victor Wanyama, itapigania huduma za mshambuliaji huyu Mbelgiji, ambaye wazazi wake ni Wakenya, dhidi ya Fulham, West Ham na Wolverhampton Wanderers.

Inasemekana waajiri wa Origi, Liverpool, pia hawajakata tamaa naye kwa hivyo huduma zake hazitapakana kwa urahisi.

Naibu wa Kane, Fernando Llorente yuko makini kuondoka Spurs baada ya kuchezeshwa dakika chache sana msimu huu.

Kutokana na hili, Spurs imekuwa ikitafuta wachezaji wanaoweza kuipa makali katika safu ya mbele. Gazeti la Telegraph linasema kwamba Origi ni mmoja wa wachezaji Spurs na kocha Mauricio Pochettino wamekuwa wakiwazia. Mshambuliaji wa West Bromwich Albion, Jay Rodriguez, ambaye aliwahi kufanya kazi na Pochettino katika klabu ya Southampton, amekuwa akihusishwa na Spurs kwa muda mrefu.

Hata hivyo, ripoti nchini Uingereza zinasema kwamba uhamisho wa Origi, ambaye anasalia na miezi 18 katika kandarasi yake uwanjani Anfield na ni kizibo cha Roberto Firmino, huenda ukawa rahisi. Mchezaji wa Bournemouth, Callum Wilson pia amehusishwa na Spurs pamoja na mvamizi wa Chelsea, Tammy Abraham, ambaye yuko katika klabu ya Aston Villa kwa mkopo.

You can share this post!

Jacob Ojee ndiye nahodha mpya wa Shujaa

Ephrem Guikan, kituko uwanjani na kero kwa mashabiki

adminleo