• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
TSC kuwaajiri walimu 5,000 wa shule za upili

TSC kuwaajiri walimu 5,000 wa shule za upili

Na WANDERI KAMAU

TUME ya Kuwaajiri Walimu (TSC) itawaajiri walimu 5,000 zaidi wa shule za upili mwezi huu, ili kusaidia kushughulikia ongezeko la wanafunzi katika shule hizo, Afisa Mkuu Mtendaji Nancy Macharia alitangaza Jumanne.

Hii ni kufuatia mpango wa serikali kuhakikisha wanfunzi wote wanaofanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) wanajiunga na shule za upili.

Akizungumza jana baada ya kumtembelea kiongozi wa ODM, Raila Odinga katika afisi zake jijini Nairobi, Bi Macharia alisema kuwa hilo linalenga kuhakikisha kwamba hakuna changamoto zozote zinazotokea kutokana na ongezeko hilo.

“Tunafahamu kwamba ongezeko la wanafunzi linamaanisha kwamba lazima majukumu ya walimu waliopo yaongezeke ili kuwashughulikia. Ni kwa hilo ambapo tume imechukua hatua ya kwanza kujaribu kuwapunguzia walimu mzigo huo,” akasema.

Bi Macharia alisema walimu hao watatumwa katika maeneo mbalimbali nchini, lakini kwa kuzingatia shule ambazo zina ongezeko kubwa la wanafunzi zaidi.

“Kuna shule ambazo zimepata wanafunzi wengi sana kuliko ilivyotarajiwa. Hizo ndizo zitakazopewa kipaumbele, ili kuhakikisha kuwa shughuli za masomo zinaendelea bila matatizo yoyote. Baadaye, tutawatuma walimu zaidi katika shule ambazo zilipata ongezeko la kadri,” akasema.

Hilo linajiri huku wadau mbalimbali wa elimu wakiendelea kutoa hisia mseto kuhusu mpango wa serikali kuhakikisha wanafunzi wote wanaomaliza shule za msingi wamepata nafasi katika shule za upili.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Wilson Sossion amekuwa akishikilia kwamba mpango huo ulipaswa kutekelezwa taratibu, ili kuhakikisha miundomsingi iliyo katika shule za upili imewatosheleza wanafunzi wote.

“Ni mpango mzuri, ila serikali ingejitayarisha mapema kwa kuimarisha viwango vya shule za upili kutosheleza idadi hiyo kubwa. Kuongeza idadi ya walimu wakati changamoto kama mazingira ya kufanyia kazi zingalipo si hatua ya kuridhisha hata kidogo, kwani haiwapi motisha walimu waliopo,” akasema Bw Sossion.

Chama kimekuwa kikishikilia kuwa ni lazima tume hiyo iimarishe mazingira ya kufanyia kazi walimu kabla ya kuwaajiri zaidi, ili kuwapa motisha katika utendakazi wao. Bw Sossion alisema hilo ndilo limekuwa likichangia kudorora kwa matokeo ya mitihani katika shule za umma.

Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA) Nicholas Maiyo aliusifia mpango huo, akisema utawapa nafasi wanafunzi werevu kutoka familia maskini.

“Ni mpango utakaopanua nafasi kwa wanafunzi ambao hawawezi kumudu karo,” akasema.

Mwanzoni mwa mwezi huu, walimu walikuwa wametishia kugoma, wakiilaumu TSC kwa kuwahamisha bila kuzingatia kanuni zilizowekwa.

Walimu vile vile walilalama kwamba, tume hiyo imekuwa ikiwanyima nafasi za kujiendeleza kimasomo, licha ya juhudi wanazoweka. Hata hivyo, pande hizo mbili zilifikia maamuzi yao nje ya mahakama.

Wadau wamekuwa wakiwaomba walimu na tume hiyo kuanza juhudi za kutatua mizozo kati yao kwa njia ya amani, ili kuhakikisha kwamba wanafunzi hawaathiriwi na mizozo hiyo.

You can share this post!

Serikali kugharimia mazishi ya afisa wa GSU aliyeuawa...

Moses Kuria aongoza wabunge wa Jubilee kuunga mkono Mawathe

adminleo