• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Moses Kuria aongoza wabunge wa Jubilee kuunga mkono Mawathe

Moses Kuria aongoza wabunge wa Jubilee kuunga mkono Mawathe

Na BENSON MATHEKA

WABUNGE kadhaa wa chama cha Jubilee wametangaza kuwa watamuunga mgombeaji wa chama cha Wiper Julius Mawathe kwenye uchaguzi mdogo wa kiti cha eneobunge la Embakasi South.

Wakiongozwa na mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, wabunge hao walisema walifikia uamuzi wao binafsi kwa sababu chama cha Jubilee hakitakuwa na mgombeaji kwenye uchaguzi huo.

Wiki jana, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alitangaza kuwa chama hicho hakitawasilisha mgombeaji katika uchaguzi huo kufuatia muafaka na uwiano nchini.

Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya ushindi wa Bw Mawathe wa chama cha Wiper kubatilishwa na mahakama.

Jana, Bw Kuria aliongoza wabunge Charles Kanyi Jaguar (Starehe), George Theuri (Embakasi Magharibi) na Simon Mbugua (EALA) kukutana na aliyekuwa seneta wa Machakos Johnstone Muthama kabla ya kutangaza kuwa watamuunga Bw Mawathe.

“Jubilee hakitawasilisha mgombeaji kwenye uchaguzi mdogo wa Embakasi Kusini. Na kwa hivyo, kwa kuzingatia muafaka na uwiano, mimi na viongozi wengine wenye mawazo kama yangu, sisi binafsi, leo tumeamua kumuunga Mheshimiwa Musili Mawathe(Wiper) kutetea kiti chake,” Bw Kuria alisema kwenye ujumbe katika ukurasa wake wa Facebook.

Bw Muthama aliandamana na mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu na Bw Mawathe. Uamuzi wa wabunge hao umepiga jeki Wiper dhidi ya chama cha ODM ambacho mgombeaji wake Irshad Sumra aliwasilisha kesi kupinga ushindi wa Bw Mawathe kwenye uchaguzi mkuu wa 2017. Chama cha Thirdway Alliance Kenya, kimemteua Dkt Angela Mwikali kuwa mgombeaji wa kiti hicho kwenye uchaguzi huo mdogo wa Aprili 5.

Kiongozi wa chama hicho, Dkt Ekuro Aukot, alisema chama hicho kimeamua kumpa tiketi ya kugombea kiti hicho.

“Tumemteua Dkt Angela Mwikali kugombea kiti cha Embakasi South kwa tiketi ya chama cha Thirdway Alliance Kenya kwenye uchaguzi mdogo wa Aprili 5 2019,” Bw Aukot alisema.

Dkt Mwikali atapambana na Bw Sumra wa chama cha ODM na Bw Mawathe wa chama cha Wiper.Wiper kimesema kitahakikisha Bw Mawathe atatetea kiti hicho.

Chama tawala cha Jubilee kilisema hakitakuwa na mgombeaji kwenye uchaguzi mdogo wa kiti hicho na kile cha Ugenya ambacho kiliachwa wazi ushindi wa Chris Karani ulipobatilishwa na mahakama.

Vyama vya Wiper na ODM vimekuwa vikilaumiana kuhusu kiti cha ubunge cha Embakasi Kusini kila kimoja kikijipiga kifua kuwa mgombeaji wake ataibuka mshindi.

Wiper kinalaumu ODM kwa kukifanya kipoteze kiti hicho licha ya vyama hivyo kuwa washirika katika muungano wa NASA, nao viongozi wa ODM wanasema muungano huo ulisambaratika.

Vyama hivyo vimewapa wagombeaji wao tiketi za moja kwa moja.

You can share this post!

TSC kuwaajiri walimu 5,000 wa shule za upili

Kaunti yatetea ziara ya Uganda iliyoigharimu Sh15 milioni

adminleo