• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
NGILA: Sheria ya utambulisho wa DNA itasaidia kuzima uhalifu

NGILA: Sheria ya utambulisho wa DNA itasaidia kuzima uhalifu

NA FAUSTINE NGILA

SHERIA mpya kuhusu Usajili wa Watu iliyorekebishwa na kutiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta kuruhusu serikali kuchukua taarifa za vinasaba (DNA) kutoka kwa Wakenya itaifaa nchi hii pakubwa.

Sheria hiyo pia itawataka wananchi kutoa taarifa kuhusu wanakoishi wanapojaza fomu za kupata kitambulisho cha kitaifa na pia Serikali sasa itatumia teknolojia ya kutambua maeneo ya GPS ili kupata makazi yao kupitia kwa setilaiti.

Hii ni hatua muhimu katika vita dhidi ya uhalifu, makosa ya jinai na ugaidi kwani taarifa kuhusu washukiwa zitaweza kulinganishwa na zile zilizoko katika hifadhi ya kitaifa ya data za DNA.

Pia hatua hii itasaidia pakubwa kutatua mizozo ya kifamilia, hasa kuhusu ugavi wa mali baada ya mabwanyenye kufariki, ambapo watoto na wanawake hujitokeza kudai kuwa ni watu wa familia ya mwendazake.

Katika vita dhidi ya uhalifu, teknolojia hii inayohusisha pia mawimbi ya sauti, alama za vidole na mchoro wa macho ya kila Mkenya na umbo la masikio, itatusaidia kuwatambua majambazi wanaohangaisha wananchi wakati wanapokamatwa.

Polisi sasa watahitajika tu kuchukua data za DNA kutoka maeneo ya uhalifu na kuwasaka washukiwa kupitia mfumo wa dijitali, kisha kuwafuatilia kupitia GPS na hatimaye kuwakamata na kuwafungulia mashtaka.

Kuanzia sasa kesi za mauaji, ufisadi, ubakaji, wizi wa mabavu, ulaghai na ugaidi hazitakosa ushahidi wa kutosha mahakamani tena kwani taarifa za DNA zitathibitisha washukiwa kuhusika kwa uovu.

Sheria hii mpya pia italeta mfumo wa pamoja wa kusimamia utambulisho wa wananchi, raia wa kigeni, wakimbizi, vyeti vya kuzaliwa na kufa, paspoti na leseni za kuendesha magari.

Kufuatia wazo hili, magari yote yanayohusika katika uhalifu yataweza kupatikana pamoja na majina ya wenyewe.

Hivyo, itakuwa vigumu kwa watu kumiliki vitambulisho zaidi ya kimoja kwani DNA ni taarifa ya kipekee kwa kila mtu na haiwezi kamwe kuwiana na ya mtu mwingine, jinsi zilivyo alama za vidole.

Wezi na wanyakuzi wa ardhi waliozoea kwenda kubadilisha hatimiliki za wenye ardhi kupitia mbinu za kidijitali pia watazimwa na mfumo huu ambao utamtaka kila Mkenya kujitambulisha kwa DNA wakati wa ununuzi na uuzaji wa mali ya fedha nyingi.

Katika ulingo wa teknolojia, mara hii serikali yetu imetumia mbinu mwafaka kukabili maovu ambayo huirudisha jamii nyuma huku haki ikikiukwa na uhalifu kuzidi kuongezeka kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha wakati kesi hizi zinasikilizwa mahakamani.

You can share this post!

WASONGA: Walinzi wapewe bunduki lakini iwe kwa masharti

Serikali yakosa kulipa wazee miezi 4 mfululizo

adminleo