• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
KCB yatoa Sh75 milioni kufadhili mbio za magari

KCB yatoa Sh75 milioni kufadhili mbio za magari

Na GEOFFREY ANENE

BENKI ya KCB imerejea katika mashindano ya mbio za magari kwa kishindo baada ya kutangaza Alhamisi itakuwa mdhamini mkuu wa mashindano ya mwaka 2019, 2020 na 2021 na kumwaga Sh75 milioni katika makala hayo matatu.

Kila mwaka, benki hiyo imesema itatumia Sh20 milioni kuandaa duru za Mbio za Kitaifa za Magari (KNRC) na Sh5 milioni kwa mashindano ya vigari vya Autocross. Fani hizi mbili sasa zitatumia majina KCB Bank Rally na KCB Bank Autocross.

Ikitangaza udhamini kwa Shirikisho la Mashindano ya Mbio za Magari la Kenya (KMSF), KCB imesema kutakuweko na duru saba za mbio za magari na duru 10 za Autocross mwaka 2019.

“Kama mdhamini wa muda mrefu, tunapenda mashindano ya mbio za magari, tunaamini udhamini wetu utaleta ladha zaidi katika fani hii,” alisema Mkurugenzi wa Mauzo na Mawasiliano, Angela Mwirigi.

“Tunaamini kwamba michezo ina nguvu ya kubadilisha maisha kwa njia nzuri. Tunaona fursa hii kama njia muhimu ya kushirikiana na jamii na kukuza talanta katika eneo la Afrika Mashariki,” alisema jijini Nairobi.

KCB inarejea kuwa mdhamini mkuu baada ya kuwa benki rasmi ya KMSF katika misimu 2016, 2017 na 2018.

“Tunafurahia udhamini huu muhimu kutoka kwa KCB. Utatusaidia sana katika kuamsha hamu ya mashindano tunapojiandaa kutumia mwaka 2019 kutafuta titketi ya kurejeshwa katika kalenda ya Mbio za Magari za Dunia (WRC),” alisema Mwenyekiti wa KMSF, Phineas Kimathi.

Mashindano ya Autocross yataanza wikendi hii ya Januari 26-27 katika eneo la Mai Mahiu yakifuatiwa na duru ya ufunguzi ya mbio za magari itakayoandaliwa katika kaunti za Nakuru na Baringo wikendi ya Februari 1-2.

You can share this post!

Family Bank yaondolewa lawama kwenye kashfa ya NYS

Serikali ilituhadaa kutufidia, walia waathiriwa wa ghasia...

adminleo