• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Afisa wa Gor awataka wachezaji kukoma kukosoa mbinu za kocha

Afisa wa Gor awataka wachezaji kukoma kukosoa mbinu za kocha

NA CECIL ODONGO

AFISA Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Omondi Aduda amewataka wachezaji wa timu hiyo kushirikiana na kocha Hassan Oktay ili kuzalisha matokeo mazuri badala ya kulalamikia mbinu zake za ukufunzi.

Katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali, afisa huyo alisikitikia taarifa zilizofichua hali halisi ya uhasama mkubwa kati ya baadhi ya wachezaji wa K’Ogalo na Oktay ambao wanadai kwamba raia huyo wa Uturuki ni mkali kwao na huwalazimishia mbinu za ‘kiajabu’ za usakataji kabumbu wasizozielewa.

“Ndiyo huenda kuna shida ila wachezaji wanafaa wafahamu kwamba kila kocha ana mbinu zake za ukufunzi. Mbinu wasiyoipendelea ya kutafuta magoli kwa kushambulia ndiyo soka ya enzi hizi kuliko soka ya zamani ya Dylan Kerr (kocha wa zamani) ya kumiliki mpira,” akasema Aduda.

Akionekana kumtetea Oktay, afisa huyo alisema kubanduliwa kwa K’Ogalo katika kipute cha Supercup jijini Tanzania Jumatano Januari 23 kulitokana na usimamizi mbovu ila akasema hiyo imewapa nafuu na muda bora wa kujitayarisha kwa mechi mbili za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) na ile ya Kombe la Mashirikisho Jumapili Februari 3 ijayo dhidi ya Zamalek ya Misri.

“Nawaomba mashabiki wetu wapunguze vamia vamia dhidi ya kocha na kumpa muda. Wakati huu klabu inahitaji utulivu wala si mambo yanayotatiza udhabiti wa timu. Ingawa nakiri mambo si ya kuridhisha kimatokeo naomba kila mtu atekeleze wajibu wake kubadilsha hali hiyo badala ya kulalamika,” akasema Aduda.

Afisa huyo veterani pia alifichua kwamba wamesajili jina la mshambulizi wa zamani wa timu ya Taifa Harambee Stars Dennis Oliech na mwenzake Geoffrey Ochieng’ kwa Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) ili waweze kujumuishwa kwenye orodha kamili ya wachezaji wanaoruhusiwa kisheria kuwajibikia kipute hicho.

You can share this post!

Wakenya watatu kushiriki Dubai Marathon

NAKURU: Walevi waungana kuwakomboa wenzao

adminleo