• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
KAHUHO TITANS: Timu iliyostawishwa kwa utu Kabete

KAHUHO TITANS: Timu iliyostawishwa kwa utu Kabete

Na PATRICK KILAVUKA

UTU ndio ulikuwa msingi na sababu cha timu ya Kahuho Titans kutoka Kahuho, kaunti ndogo ya Kabete, Kaunti ya Kiambu kubuniwa.

Kocha wake Francis Mwaura alijitokeza na wazo la kujenga timu hii baada ya kuona mawimbi ya maisha yakianza kusomba vijana ambao wana vipaji adimu vya wanasoka kupitia mambo ya utovu wa nidhamu na usalama na akaamua kujitokeza na wazo la kuwaweka katika mkondo wa kukuza talanta zao na kunidhamishwa. Mbali na kuwanusuru kutokana na janga la mihadarati.

Kikosi cha Kahuho Titans kutoka Kahuho, kaunti ya Kabete kikipasha misuli moto .Picha/Patrick Kilavuka

Kwa kuthamani kabumbu maana mwenyewe, amekuwa akisukuma gurudumu la kandanda akichezea timu mbalimbali kabla kuchukua mikoba ya ukufunzi, anasema aliamua liwe liwalo azma yake ya kutetea vipawa vya kandanda haitazima ila, atapiga jeki wanasoka waliolivalia njugu suala la kusakata boli kuafikia malengo yao kupitia ukufunzi.

“Kabla nivae jezi la ukocha, nilikuwa nimechezea timu ya makinda ya Kahuho Junior, Kahuho Senior FC kabla kusajiliwa na timu ya Umoja, Kanjeru halafu kuwindwa na Shambani FC ya Voi.

Kikosi cha wapinzani Cuba Stars kutoka Nyathuna, kaunti ndogo ya Kabete. Picha Patrick Kilavuka

Hii ni baada ya kocha wa timu hiyo kuhudhuria ngarambe ya Bonanza ambayo ilikuwa imeandaliwa Ngichirani- Gikambura, kaunti ya Kabete na muandalizi Sanyo na jicho pevu la kocha wa timu hiyo ya Voi likanilenga mwaka 2013,” aeleza kocha Mwaura na kuongezea kwamba, alipata kuihudumia timu hiyo kwa miezi mitatu kabla kurudi nyumbani na kuwazia kusaidia wanasoka chipukizi.

Mkufunzi Mwaura aliasisi timu hii mwaka wa 2014. Kwa sasa, timu ina wachezaji 32 ambao wanajitahidi ukucha kwa jino kupiga msasa vipaji vyao na kuinuia viwango vyao vya kandanda kwa kupiga mazoezi Jumanne hadi Jumamosi uwanja wa Shule ya Msingi ya Kahuho iwapo hawana gemu au wanafanya maandalizi ya mchuano.

Kocha Mwaura anasema kwamba, kwa kuyaelewa mazingira ambayo vipawa vya wanadinga hawa vinakuziamo, kumempa kazi rahisi ya kuwakuza.

Isitoshe, kumejenga daraja bora ya kuwapa mafunzo kwani wamekuwa wajitokeza kwa moyo mkungufu kufanya mazoezi na kuwa radhi kujifunza ili wajiongezea maarifa, kushirikiana na kuuwiana wao kwa wao.

Kando na hayo, umoja umezidisha upendo timuni na wanatiana moyo katika kutoa ushindi dhidi ya wapinzani wao licha ya changamoto kuwapo.

Cha mno kibakiayo kwake kama kocha, anasema ni kuwahimiza tu kuendelea kufuatilia maono yao ndiposa wayaona matunda ya bidii yao.

“Napigwa moyo konde na wachezaji hawa ambao wana mori ya kupigana kiume na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu sana wakishuka mchezoni huku wanavuna ushindi au wapotezapo hurudi kwenye ubao kujitafuta upya kurekebisha dosari za mechi tangulizi.”

“Pia, huwa wako huru kueleza kama kuna jambo ambalo linaenda ndivyo sivyo kambini ili, timu iimarishwe pasi na kuchukiana au kudharauliana,” aeleza kocha huyo na kuongezea kwamba, migorogoro ya timu nyingi inasababishwa na kocha kuonea wachezaji au kuwachukia hali ambayo hushusha ari ya wachezaji na matokeo kuwa mabaya.

Hata hivyo, siri ya timu yake imekuwa kuwapa sikio wachezaji wake na kuwaelekeza anakoona kamba inalegezwa kuhimili timu kufanya kazi njema.

Wachezaji hawa hupokea huduma ya kwanza kuhakiksha kuwa wanapata afueni kutokana na majeraha madogo madogo kama njia ya kuzingatia afya yao.

Isitoshe, imekumbatiwa na mashabiki ambao wanaiandama kila wakati wanacheza mechi na hata hujitolea kuchangia timu ndiposa isikose nauli wala ada ya marefa.

Wachezaji wake hupenda kufuata maagizo ya mpuliza kipenga. Pia, kupitia unahodha mzuri wa Stanely Njuguna wanatiwa katika barabara ya nidhamu na kutandaza soka safi na ya kutamanika.

Kapteni Njuguna, huwahimiza wachezaji kujiepusha na dhoruba ambazo zinaweza kuzua mchafuko uwanjani kwa kudumisha amani na kucheza mchezo usiokuwa na ngware wala majeruhi kwa wengine na kusalimana ishara ya kudumisha amani.

Pia huyapa maombi kipaumbele kabla ya mpepetano na baada ya mchuano kutamatika kama njia ya kumshukuru Maulana mpaji vipaji, nguvu na neema ya afya.

Chini ya uongozi wa kocha Mwaura na msaidizi Kariuki timu imeshiriki vipute na Ligi ya Kabete.

Imeweka kabatini taji la Mwakilishi wa eneo la Kahuho Eluid Ndithia mwaka 2018 na kutunukiwa kombe, sare na mipira mitatu.

Wao si wachache katika mchakato wa ligi ya Kabete kwani makali yao huhisiwa.

Mwaka wa 2015, timu ilifika fainali na kushinda taji baada ya kuchapa Blackslates 2-0 katika uga wa Mukoi.

Mnamo 2016, walifika nusu fainali na kupoteza dhidi ya Congo Boys ambao waliwararua 2-1 uwanja wa Chuo cha Kiufundi cha Kamuguga.

Mwaka 2017, meli yao ilitua nanga katika nusu fainali baada kukubali kichapo cha 1-0 kutoka kwa mahasimu wao Euronuts uwanja wa Shule ya Msingi ya Uthiru.

Msimu wa 2018-2019, wameteremka dimbani mara tano.

Katika michuano hiyo, walishindwa kwa ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Euronuts FC, kutoka sare tasa dhidi ya Congo Boys na kuibwaga LA 2-0.

Matokeo mengine, waliishinda Bayern 1-0 na juzi, walizima Cuba Stars 2-0 uwanjani Kanjeru na hivyo basi kujikisanyia alama 10.

Kikosi kinajumuisha kipa Antony Kariuki, Morris Kimani, Simon Kamau, Peter Ngugi, James Karanja, Stanely Njuguna (kapteni), Andrew Kimengi, Dedan Njoroge, Alex Gitau, Ken Njoroge na Julius Thiongo.

Wengine ni Caxton Mburu, Mustafa Ali, Paul Nganga na kadhalika.

Kuimarisha kikosi zaidi, kocha Mwaura amesajili wanasoka Mustafa Ali kutoka klabu ya Blackslates na Paul Nganga kutoka Cuba Stars.

Mipango? Kulingana na mwalimu wao, wananuia sasa kujikasa kisabuni kujitosa katika ligi ya daraja ya Pili -Kabete, kisha ile ya Silver kisha kuyoyomea ya Kaunti ya Kiambu majaliwa. Pili, kupambana na changamoto za timu kusukuma gurudumu lake zikiwemo za ufadhili.

You can share this post!

Korti yakubali ushahidi kuhusu shamba la Sh8 bilioni...

Presha kwa Shujaa katika michuano ya Hamilton Sevens

adminleo