• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
Tutaonyesha Raila kivumbi Embakasi – Wiper

Tutaonyesha Raila kivumbi Embakasi – Wiper

WYCLIFFE MUIA na KITAVI MUTUA

KINARA wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameapa kumuonyesha kivumbi Raila Odinga katika uchaguzi mdogo wa Embakasi Kusini, iwapo kinara huyo wa ODM hatamuondoa mwaniaji wake Irshad Sumra katika kinyang’anyiro hicho cha Aprili 5.

Bw Musyoka alisema itakuwa aibu sana kwa Bw Odinga na yeye kumenyana hadharani katika kampeni za marudio ya uchaguzi huo, licha ya kuwepo na ‘handisheki’ iliyotuliza joto la kisiasa nchini.

“Iwapo ODM haitakubali kuondoa mgombeaji wake, nawahakikishia kuwa wataona kivumbi. Mimi mwenyewe nitakuwa pale kumfanyia kampeni mwaniaji wa Wiper,”alisema Bw Musyoka baada ya kumkabidhi cheti mwaniaji wa Wiper Julius Mawathe jana.

Makamu huyo wa Rais wa zamani alisema tabia ya NASA kuwa na wagombeaji wengi katika uchaguzi mmoja ndio ilipelekea muungano huo kupoteza viti vingi bungeni katika uchaguzi uliopita.

“Huu ndio wadhifa wa pekee wa ubunge Wiper imeshikilia jijini Nairobi na hatuwezi kukubali kunyang’anywa. Iwapo muungano wa NASA unaamini kuwepo na umoja, unapaswa kuachia Wiper kushikilia huu wadhifa,”alisema Bw Musyoka.

Bw Musyoka alisema tayari chama cha Ford Kenya kinachoongozwa na Seneta(Bungoma) Moses Wetangula kimetangaza kuunga mkono Wiper katika marudio ya uchaguzi huo.

“Naamini chama cha ANC pia hakina mwaniaji na nitashauriana na kinara wake Musalia Mudavadi pia aunge Wiper mkono.”

Tayari chama cha Jubilee kimesema hakitakuwa na mwaniaji katika uchaguzi huo mdogo huku baadhi ya wabunge wake wakiapa kuunga mkono mwaniaji wa Wiper.

Ushindi wa Bw Mawathe ulifutiliwa mbali na Mahakama ya Rufaa baada ya mpinzani wake wa ODM Irshad Sumra kuupinga akilaumu Tume ya Mipaka na Uchaguzi(IEBC) kwa kumnyima ushindi katika uchaguzi wa 2017.

IEBC ilitangaza Bw Mawathe mshindi mnamo 2017 kwa kupata kura 33,880 dhidi ya Bw Sumra aliyepata kura 33,708.

Jana, Bw Musyoka alisema Mawathe atahifadhi wadhifa wake kwa zaidi ya kura 50,000.

“Nawarai waajiri wawape wapiga kura wa Embakasi Kusini nafasi ya kushiriki mchakato huu muhimu wa kidemokrasia,”alisema Bw Musyoka.

Wiki iliyopita, aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama alikutana na wabunge wa Jubilee wanaounga Wiper na akaambia ODM kuwa tayari kwa ushindani mkali katika uchaguzi huo mdogo

Bw Muthama alikutana na wabunge wa Jubilee; Moses Kuria (Gatundu Kusini), George Theuri (Embakasi Magharibi), Simon Mbugua (EALA), Charles Kanyi (Starehe) na Makali Mulu (Kitui ya Kati) ambao waliapa kuhakikisha Bw Mawathe amehifadhi kiti hicho.

Wakati huo huo, Bw Musyoka jana alifanya kikao cha faraghani na viongozi wa Ukambani nyumbani kwake Yatta, Kaunti ya Machakos kujadili hatima ya mwenyekiti wa Wiper Prof Kivutha Kibwana.

Prof Kibwana amekuwa akitofautiana na baadhi ya maamuzi ya Bw Musyoka haswa baada ya kutangaza kuwa ‘mtu wa mkono’ wa Rais Uhuru Kenyatta.

Gavana huyo wa Makueni sasa ameungana na wenzake Charity Ngilu(Kitui) na Dkt Alfred Mutua(Machakos) kupinga uongozi wa Bw Musyoka eneo la Ukambani na kuapa kutoa ‘sura mpya’ ya siasa za eneo hilo.

You can share this post!

Nyanya wa miaka 81 abakwa, amwagiwa asidi kisha kuuawa

Ufisadi umekita mizizi Kenya – Ripoti

adminleo