• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Joho atetewa kuhusu madai ya mihadarati

Joho atetewa kuhusu madai ya mihadarati

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE watatu wa ODM Jumatano walipuuzilia mbali madai ya Gavana wa Nandi, Stephen Sang’ kwamba mwenzake wa Mombasa, Ali Hassan Joho anahusika katika biashara ya dawa za kulevya huku wakimtaka kuwasilisha ushahidi kwa polisi kuthibitisha madai yake.

Wakiwahutubia wanahabari jana katika majengo ya bunge, watatu hao, Abdulswamad Nassir (Mvita), Mishi Mboko (Likoni) na Babu Owino (Embakasi Mashariki) pia walitaja kama uvumi madai kwamba Gavana Joho amezimwa kuzuru Amerika kutokana na uhusiano wake na ndugu wawili wa Akasha, ambao wamekiri mashtaka ya ulanguzi wa mihadarati.

“Tunatoa changamoto kwa Gavana Sang na wenzake wanaoeneza madai hayo ya uwongo kuwasilisha ushahidi wowote walio nao kwa polisi,” akasema Bw Nassir.

Alisema Bw Joho amekuwa akizuru Amerika kila mara bila vikwazo vyovyote tangu Kaunti ya Mombasa ilipoanzisha ushirikiano na jiji la Seattle.

Agosti mwaka jana, Bw Joho alizuru jiji kuu la Amerika, Washington, kuhudhuria mkutano wa kujadili ongezeko la visa vya mashambulio ya kigaidi katika eneo la Pwani chini ya mwavuli wa mpango wa Strong Cities Network.

Mnamo Jumapili, Gavana Sang’ alidai Bw Joho amekuwa akiwahadaa Wakenya kuhusu muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.

“Joho ni kiongozi ambaye amewapotosha vijana wengi katika eneo la Pwani ambako wengi wao wamekuwa mateka wa dawa za kulevya, biashara ambayo yeye Joho huendesha,” akasema Bw Sang’ alipowahutubia waumini katika kanisa la St Francis of Assisi Cheptarit, katika Kaunti ya Nandi.

Bw Sang’ alisema ni makosa kwa Bw Joho kudai kuwa anaunga mkono muafaka huo ilhali anampiga vita Naibu Rais William Ruto.

Alionekana kukerwa na madai ya Bw Joho wiki jana akiwa Kaunti ya Busia kwamba atafanya kila awezalo kumzuia Dkt Ruto kuingia Ikulu.

“Naibu Rais Dkt Ruto alichaguliwa pamoja na Rais Kenyatta. Kwa hivyo, haifai kwa Joho kusema kuwa anaunga mkono Rais lakini anampinga naibu wake. Hapo anawachezea shere Wakenya,” akasema Bw Sang’.

You can share this post!

Mwanamke kizimbani kwa kumlazimishia mvulana uroda

WAZIRI KIGEUGEU: Atapatapa kuhusu maamuzi ya uchukuzi

adminleo