• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
SOLAI: Makabiliano ya polisi na wakazi wanaotaka fidia baada ya mkasa

SOLAI: Makabiliano ya polisi na wakazi wanaotaka fidia baada ya mkasa

NA RICHARD MAOSI

WAKAZI wa eneo la Solai, Kaunti ya Nakuru Jumatano walikabiliana na polisi walipozuiliwa kuhudhuria mkutano wa amani ulioratibiwa na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KHRC).

Jamaa za familia walioathirika na mkasa wa bwawa la Solai ambalo lilivunja ungo na kusababisha maafa ya watu zaidi ya 40, walilalamika kutengwa na serikali licha ya ahadi nyingi kutolewa.

Miezi tisa baada ya tukio walioathiriwa hawakuwa wamepata fidia huku madai mapya yakizuka kuwa ni viongozi wa kaunti walikuwa wamewapunja.

Mwanamume abeba mawe kufunga barabara. Picha/ Richard Maosi

Kiongozi wa wadi ya Kabazi BW Peter Mbai aliyaongoza maandamano, huku akiwaleta pamoja wakazi wenye hasira.

Kwa ushirikiano na katibu mkuu wa KHRC nchini George Kegoro aliyefika kuhutubu, mkutano huo ulifanyiwa maandalizi lakini haukufanyika.

Maafisa wa KHRC walikuwa wameandaa mkutano wa kuwahamasisha wakazi, kuhusu haki zao lakini siku ya tukio walikuta eneo lenyewe limezingirwa na walinda usalama walioshika doria.

Moto uliowashwa na waandamanaji. Picha/ Richard Maosi

Viongozi wa usalama walisema hafla iliyoandaliwa haikuwa halali ndipo wakawatawanya wakazi wakitumia vitoa machozi.

Vijana wenye hasira walichukuwa mawe na kuyaweka barabarani wakiimba nyimbo za kudai haki yao.

Usafiri ulitatizika magari yakilazimika kuchukua njia mbadala, waandamanaji wenye fujo waligeuza ukumbi jukwaa la mchezo wa paka na panya.

Vijana wenye hasira wakiwweka mawe katikati ya barabara. Picha /Richard Maosi

Polisi walitumia nguvu kupita kiasi, kisha wakaanza kurushiwa mawe katika magari yao.

Shule jirani ya msingi ya Nyakenywa ilisitisha masomo baada ya polisi kurusha vitoa machozi ndani ya shule na kuwatia hofu wanafunzi waliokuwa wakiendelea na masomo .

“Hatutaondoka hapa hadi tufahamu fidia ya watu wa Solai iko wapi. Tungependa kujadiliana kama wakazi wa Solai lakini polisi wasiokuwa na utu wanatuhangaisha,” Bw Mbai alisema.

Mwanahabari akitimua mbio baada ya kurushiwa kitoa machozi katika mshikemshike wa polisi na raia. Picha/ Richard Maosi

Kutokana na hasira za wakazi, mali ya Patel yalitiwa moto na kuchochea mapambano zaidi kati ya polisi na raia.

“Tumeshuhudia kwa macho yetu leo, kuwa bado tunaishi katika enzi za kikoloni,” Bw Kegoro alisema.

Umma ilishuhudia shamba pamoja na msitu unaokuza miti ya mwekezaji Patel ikiteketezwa.

Katibu mkuu wa KHRC George Kegoro akiwafokea polisi waliojaribu kumtia kuzuizini. Picha/ Richard Maosi

Kwa mujibu wa mzee wa mtaa John Mwangi, alikuwa tayari kupoteza maisha yake akiwatetea wanakijiji wake.

Akiwa mkulima wa kahawa anasema shamba lake lilikuwa limefurika mlima wa mchanga uliosombwa na maji siku ya mkasa.

Kwa sababu msimu wa kupanda kahawa ulikuwa umefika ,hakuwa ameona dalili yoyote ya serikali kumfidia wala kumsaidia alainishe shamba lake, anapojiandaa kupanda.

Polisi wakiwa wameimarisha usalama dhidi ya waandamanaji waliotaka kuhudhuria mkutano. Picha/Richard Maosi

Aliungwa mkono na mwenzake Steve Mwangi aliyeeleza Taifa dijitali kwamba hizi zilikuwa ni hatua za mwisho wakielekea kupata suluhu ya kudumu.

“Tulikuwa tumepata idadi kamili ya waathiriwa na ajenda yetu kubwa ilikuwa ni kupata mwafaka baada ya mazungumzo yetu na Patel kushindikana,” alisema.

Hii ilikuwa ni siku ya mwisho kuandikisha watu kabla ya kuanzisha upya mchakato wa fidia mahakamani kumshataki Patel na waliofyonza fidia yao.

Polisi wakitumia vitoa machozi kuwatimua wakazi waliokuwa wakijiandaa kabla ya kuhudhuria mkutano ulioandaliwa na shirika la Human Rights Solai. Picha/Richard Maosi

“Wakazi tulikuwa tunazungumza kwa sauti moja baada ya kugundua hatukua karibu na kupata msaada,” alisema.

OCPD wa Rongai alisema swala la Solai lilikuwa limeingizwa siasa nyingi na kutatiza makubaliano.

“Itabidi polisi wavalie njuga swala hili kwa kina uchunguzi ukiendelea, lakini wote waliochochea ghasia hawataepuka mkono wa sheria,” alisema.

Vitoa machozi vyajaa hewani. Picha/ Richard Maosi

 

Waathiriwa wa mkasa walikuwa wamejaribu kuzungumza na mmiliki wa bwawa Mansukul Patel bila mafanikio.

Inasemekana Patel aliwageuka siku za hivi karibuni akisema hakuwa akiwatambua.

Kwa sababu alikuwa na kesi mahakamani alisema hakuwa na wakati wa kuzungumza na walalamishi.

Baadhi ya vijana waliozua ghasia walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Rongai,wakisubiri kuandikiwa mashataka dhidi ya uharibifu wa mali na kutatiza utulivu.

Wengi walitazama makabiliano kwa umbali. Picha/ Richard Maosi

Aidha maduka yalibakia kufungwa kwa siku nzima wauzaji wakirejea nyumbani mapema.

Baadhi yao waliibiwa bidhaa wakiandikisha hasara kutokana na kundi kubwa la vijana ambao hawangeweza kuzuilika.

“Nilikuwa nikiwahudumia wateja wangu kundi la vijana waliokuwa wamejihami kwa mawe walipovamia duka wakitaka soda,maziwa na maji,” alisema Nancy Chege muuzaji katika duka la kijumla.

Polisi wakikabiliana na waandamanaji katika operesheni ya kurejesha utulivu katika eneo la Solai Nakuru. Picha/Richard Maosi

Mkasa wa Soali ulisomba nyumba nyingi katika kijiji cha Nyakenyua pamoja na shule mnamo Mei 2018.

Watu 48 walidhibitishwa kupoteza maisha yao wengi wakiwa ni watoto.

Waziri Matian’g alitembelea eneo la tukio na kusema huenda maafa yalikuwa zaidi ya 48 kwani baadhi ya watu walizikwa na mafuriko.

Mmiliki wa Patel alizungumza baada ya siku sita kwa kuwapatia pole waliopata hasara huku akipongeza juhudi za serikali katika shughuli nzima ya uokozi.

Baadhi ya makuburi ya waathiriwa wa mkasa wa Solai Nakuru mnamo Mei 2018. Picha/Richard Maosi

Rais Uhuru Kenyatta pamoja na naibu wake William Rutto walitembelea eneo la tukio siku ya misa ya wafu na kuahidi kuwafidia.

Baadaye Kenya Water Resourses and Management Authority (WARMA) walifanya uchunguzi na kugundua bwawa la Solai halikuwa na kibali cha kuendesha shughuli kwa kutozingatia usalama.

Baadaye kutokana na shinikizo la umma wamiliki wa bwawa la Solai walijisalimisha katika mahakama ya Naivasha wakikabiliwa na mashataka ya mauaji ya halaiki..

You can share this post!

Hoteli za kifahari Pwani zapiga marufuku chupa za plastiki

UKEKETAJI: Juhudi zilizochangia tohara ya wanawake kupungua...

adminleo