• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
Ruto kujadili suala la marekebisho ya Katiba Uingereza

Ruto kujadili suala la marekebisho ya Katiba Uingereza

Na VALENTINE OBARA

NAIBU Rais William Ruto amepata mwaliko Uingereza kujadili kuhusu suala tatanishi la marekebisho ya katiba nchini.

Dkt Ruto anatarajiwa katika taasisi mashuhuri ya utafiti wa sera za uongozi ya Chatham House iliyo jijini London Ijumaa. Taasisi hiyo inafahamika sana kwa kualika viongozi mbalimbali kuzungumzia masuala ya siasa na utawala.

“Huku Kenya ikikaribia kukamilisha muongo mmoja tangu kupitisha katiba mpya mwaka wa 2010, bado kuna changamoto ya kutambua uhalisia wa athari za kisiasa na kiuchumi za mabadiliko yaliyofanywa,” inasema sehemu ya maelezo kuhusu hafla hiyo.

Inaongeza, “Kwa kuzingatia miito ya mabadiliko zaidi ya katiba ambayo yanasababisha mgawanyiko kwa Wakenya wengi, ni muhimu kwamba mafunzo yaliyopatikana katika kipindi cha muongo mmoja uliopita yatumiwe kuamua hatua itakayochukuliwa na nchi.”

Dkt Ruto alikuwa miongoni mwa waliopinga katiba ya 2010 na katika siku za hivi majuzi, amekuwa pia akipinga mapendekezo ya kuirekebisha isipokuwa kama mabadiliko yatahusu uimarishaji wa ugatuzi.

Suala la kura ya maamuzi limekuwa likigonga vichwa vya habari tangu Rais Uhuru Kenyatta alipoungana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuleta umoja wa kitaifa kupitia kwa jopo maalumu ambalo linaendelea kukusanya maoni ya wananchi.

Ingawa Chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Odinga kimeeka wazi mapendekezo yake kutaka kuwe na rais asiye na mamlaka makubwa na badala yake kuwepo Waziri Mkuu mwenye mamlaka makuu, chama tawala cha Jubilee kilisema wanachama wake wako huru kujiamulia wanachotaka kuhusu marekebisho hayo yanayojadiliwa.

Uamuzi wa Jubilee ulionekana na wachanganuzi wa kisiasa kama mkakati wa kuzuia mgawanyiko zaidi chamani kwani mdahalo huo wa kura ya maamuzi ulikuwa tayari umesababisha uhasama kati ya wandani wa Dkt Ruto na baadhi ya wanachama kutoka Mlima Kenya.

Wandani wa naibu rais wanaamini marekebisho yanayopigiwa debe ni njama ya kuvuruga mipango yake kushinda urais ifikapo mwaka wa 2022.

Msimamo wa Dkt Ruto umekuwa kwamba ataunga mkono marekebisho ya katiba ikiwa tu yataimarisha ugatuzi kwa minajili ya kustawisha maendeleo kwa manufaa ya raia.

“Ugatuzi ulibuni serikali 47 za kaunti ambazo zinaweza kusaidia kupanua biashara, uwekezaji, kuongeza nafasi za ajira na mapato lakini serikali nyingi za kaunti zimekuwa zikitatizika kupata kiwango cha kutosha cha mapato,” taarifa ya Chatham House ikasema.

Iliongeza, “Katika hafla hii, Dkt Ruto atazungumzia changamoto za kusimamia mabadiliko katika nchi yenye misimamo tofauti tofauti, na kutabiri hali itakavyokuwa Kenya katika siku zijazo na vile vile barani.”

Mnamo Jumapili wakati alipokuwa katika Kanisa Anglikana la St Paul’s eneo la Naragwa, Kaunti ya Nyandarua, viongozi walioandamana naye walizidi kusisitiza hawataunga mkono marekebisho ya katiba yanayonuia kubuni nafasi zaidi za uongozi.

You can share this post!

Mzazi mwanamke afukuzwa shuleni kwa kuvaa long’i

Mwanamume taabani kwa kujifanya mkewe Ruto

adminleo