• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Matiang’i aanza kazi mpya kama mkuu wa mawaziri

Matiang’i aanza kazi mpya kama mkuu wa mawaziri

Na WYCLIFFE MUIA

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i Jumanne aliongoza kikao chake cha kwanza cha Baraza la Mawaziri baada ya uteuzi wake kusimamia mawaziri katika utekelezaji wa miradi ya serikali.

Kikao hicho kilichofanyika katika jumba la Harambee, Nairobi kilihudhuriwa na mawaziri wote pamoja na Mkuu wa Sheria Kihara Kariuki na Mkuu wa Utumishi wa Umma Francis Kinyua.

Mkutano huo ulioanza saa moja asubuhi ulipangwa wiki iliyopita na mawaziri wote wakatakikana kuhudhuria kupitia afisi ya Bw Kinyua.

“Kamati Kuu ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ilifanya mkutano wake leo kutathmini miradi ya serikali. Kama ilivyoamrishwa na Rais Uhuru Kenyatta, kamati hii imetambua baadhi ya changamoto zinazoathiri miradi ya maendeleo,” ilinukuu taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho.

Bw Kibicho alisema kamati hiyo itatoa ripoti ya kila wiki kwa Rais Kenyatta pamoja na mapendekezo ya kutekeleza miradi ya serikali.

Dkt Matiangi alipewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa miradi ya serikali kisha atoe ripoti kwa rais, hatua ambayo ilizua joto katika chama cha Jubilee.

Chini ya Amri ya Rais nambari 1 ya 2019, Dkt Matiang’I anatarajiwa kuhakikisha mawaziri wote wametekeleza miradi katika wizara zao na kutoa ripoti kwake kila wiki.

Katika amri hiyo iliyotolewa Januari 21, Makamanda wa Kaunti vilevile wanapaswa kuongoza kamati za maendeleo katika maeneo yao kisha kutoa ripoti ya kila wiki kwa Dkt Matiang’i.

Wakati huo huo, Naibu Rais William Ruto jana alipokea ripoti ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka maeneo kame nchini.

Miradi hiyo inayotekelezwa na Benki ya Dunia kwa kima cha Sh200 bilioni inalenga sekta za elimu, maji, kawi, barabara na ufugaji.

Dkt Ruto alipokea ripoti hiyo afisini kwake Karen, Nairobi kutoka kwa Mkurugenzi wa Benki Kuu nchini Felipe Jaramillo, hafla iliyohudhuriwa na magavana kutoka kaunti 11.

You can share this post!

Joho awashtaki wandani wa Ruto kwa kumhusisha na mihadarati

Visa vya mauaji ya abiria wa teksi vyazua wasiwasi

adminleo