• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
NGILA: Juhudi ziongezwe kuzima ukeketaji wa siri

NGILA: Juhudi ziongezwe kuzima ukeketaji wa siri

NA FAUSTINE NGILA

FEBRUARI 6 kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Uhamasisho kuhusu Ukeketeji ambapo Umoja wa Mataifa huhimiza jamii zote kuimarisha vita dhidi ya utamaduni huu.

Ingawa Kenya imepiga hatua katika juhudi za kutokomeza uovu huu, bado kuna jamii ambazo zinaamini lazima msichana atahiri ili awe ‘mtu mzima’ pamoja na sababu zingine za kiajabu.

Uovu huu huwaletea waathiriwa magonjwa na hatimaye kufariki, lakini licha ya mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana na serikali kuhamasisha jamii husika, bado unafanywa, ila kwa siri.

Tunapoadhimisha siku hii, tunafaa kukumbuka kuwa ukeketaji ni tatizo linalokumba mataifa mengi duniani, na mbinu pekee ya kuuzima ni kubuni mbinu mbadala za kutambulisha kuvuka rika kwa wasichana wetu.

Vita dhidi ya ukeketaji vinafaa kubadilishwa. Hauwezi kutatua tatizo iwapo tatizo hilo ni kitendo kinachofanyika gizani. Uwezo wako wa kukitambua ni finyu.

Mashirika ya kupambana na ukeketaji yanafaa kubuni mtandao wa mawasiliano na watu wengi katika vijiji vya mashinani ili kupata ripoti kuhusu wanaotekeleza unyama huu.

Ukeketaji si changamoto ya jamii fulani za humu nchini. Utafiti unaonyesha kuwa yamkini kila kabila la Kenya linatekeleza ukeketaji ila taarifa hizi husalia vigumu kuzipata.

Kampeni dhidi ya imani hii zinafaa kufanywa pia katika kaunti ambazo zinaonekana kama zisizowakeketa wasichana. Cha muhimu ni kila mwananchi kuelewa kuwa ukeketaji upo, ni uovu na ni ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Hii itasaidia watu wa jamii moja kuwakosoa wenzao wa jamii inayotekeleza tohara ya wanawake.

Mbinu mbadala zimekuwa zikitumika katika mataifa kadha. Wasichana wanapopelekwa unyagoni, wasifunzwe kuhusu utumwa wa kuolewa mapema wala kukeketwa, waelimishwe kuhusu haki zao za kimsingi kama afya na elimu ambazo wakikosa, huenda maisha yao yakasambaratika.

Tatizo kuu katika vita hivi hapa Kenya vimekuwa ukosefu wa usalama katika kaunti ambako ukeketaji hufanyika zaidi, huku wakeketaji wakivuna malipo ya huduma zao.

Nimebaini kuwa kukeketa msichana mmoja ni Sh3,000 na baadaye huozwa baada ya wazazi kupokea mahari ya mbuzi 50, ng’ombe 30 na ngamia 10.

Iwapo ukeketaji utatokomezwa, pia visa vya wizi wa mifugo vitakoma kwa sababu baadhi ya wanaume wakifikia umri wa kuoa hulazimika kuiba mifugo ili walipe mahari.

Wizara ya Usalama inafaa kutoa usalama wa kutosha kwa wahamasishaji mashinani ambako utamaduni huo unaendeshwa kisiri. Hilo litatoa nafasi kwa mashirika kuwapa wakeketaji mafunzo kuhusu mbinu mbadala za kupata riziki.

Wizara ya Afya nayo iimarishe Bodi ya Kitaifa ya Vita Dhidi ya Ukeketaji, kwa kuongeza ufadhili na nguvukazi kwa kampeni dhidi ya tohara hii.

You can share this post!

WASONGA: Tulimpa Uhuru mamlaka, mbona awalilie wananchi...

KAULI YA WALIBORA: Fasili ya neno ‘binamu’...

adminleo