• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wezi watumia mabomba ya kinyesi kuiba hela benki

Wezi watumia mabomba ya kinyesi kuiba hela benki

MASHIRIKA Na PETER MBURU

WEZI nchini Ubelgiji walishangaza taifa na ulimwengu baada ya kutumia mitaro na mabomba ya maji taka na kinyesi kusafiri hadi benki moja, ambapo waliiba pesa zisizojulikana kiwango chake.

Wezi hao wanasemekana kutumia mabomba hayo, ya upana wa sentimita 40 kupitia chini ya ardhi hadi eneo ambapo pesa zinahifadhiwa katika benki iliyo karibu na wilaya ya Antwerp Diamond Trading.

Polisi walifahamishwa kuhusu tukio hilo na walipofika eneo panapohifadhiwa pesa ndani ya benki hiyo, japo mlango ulikuwa umefungwa, boksi 30 za pesa zilikuwa zimeibwa.

Hata hivyo, bado polisi hawajatangaza kiwango cha pesa ambacho wezi hao waliondoka nacho.

Maafisa wanaosimamia maji na usafi wa mazingira mji huo, hata hivyo, walisema kuwa wezi hao walihatarisha maisha yao sana kwa kutumia mbinu hiyo.

“Kwanza kabisa, kuchimba shimo ili kutokezea katika mabomba ya kusafirisha uchafu ilikuwa hatari kwani kulikuwa na uwezekano wa ardhi kuporomoka. Ndani ya mabomba hayo ya uchafu, kuna hatari nyingi kama hewa chafu inayotoka ndani ya uchafu huo,” akasema Els Liekens, wa kampuni ya maji.

Wateja wa benki hiyo walighadhabishwa na hali ya benki kutowafahamisha kuhusu kisa chenyewe, wengine wakidai kuwa boksi hizo zilikuwa zimehifadhi hazina zao za maisha.

“Watu wengi hawahifadhi pesa na vifaa vya utajiri pekee, bali pia vitu vya kifamilia,” akasema mmoja wao.

Wizi wa aina hiyo ambao ulitokea nchini Ufaransa mnamo 1976 uliwafanya wezi kuishi kwa miezi wakichimba ndani ya mabomba ya kusafirisha uchafu, kisha baadae wakaiba mamilioni ya pesa pamoja na mali iliyokuwa ndani ya boksi 200.

You can share this post!

Afueni kwa mzee aliyefungwa kwa unajisi jaji kusema watoto...

‘Aliyefanya ngono’ na BMW ajitetea kortini...

adminleo