• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
KAYOLE: Kundi lililojitolea kubadilisha taswira kuhusu mtaa

KAYOLE: Kundi lililojitolea kubadilisha taswira kuhusu mtaa

Na PAULINE ONGAJI

JE, ni nini kinachokujia akilini mtaa wa Kayole, Nairobi unapotajwa? Pengine ni visa vingi vya uhalifu, au kikundi haramu cha Mungiki, au vijana waliozama katika matumizi ya mihadarati, na hata, taswira ya mtaa uliojaa uchafu kutokana na mrundiko wa taka?

Ikiwa hiyo ndio taswira yako ya mtaa huu, basi bila shaka unahitaji kubadili mtazamao wako kwani mambo yamebadilika.

Mabadiliko haya yametokana na jitihada za kikundi cha Transform Kayole Youth, ambacho kimejitwika jukumu la kubadilisha sio tu jina, bali sura ya mtaa huu.

Chini ya uongozi wa Bw Samuel Omare, afisa mkuu mtendaji, Bi Naliaka Kupara ambaye ni karani, Bw Samuel Odamo anayehudumu kama mratibu na Bw Jibril zigo ambaye ni mweka hazina, kikundi hiki kimeunganisha vikundi vidogo vya vijana mtaani huu ili kuleta mabadiliko.

Kwa ubia na mashirika mengine ikiwa ni pamoja na Public Space Network, UN Habitat, One Stop Youth Center na Baraza la Kaunti ya Nairobi, wameunda shindano kwa jina Changing Faces Competition.

Baadhi ya sehemu ambazo ziko katika harakati za kufanyiwa mabadiliko. Picha/ HISANI

Katika shindano hili, vikundi hivi vinashindania taji kubaini ni kipi kinachopiku vingine kwa kubadilisha, kupanda miti, vile vile kusafisha majaa ya taka na kuwa mabustani, maeneo ya kuegesha magari na sehemu za kutulia.

Vikundi hivi hasa vinajumuisha vijana waliokuwa wakihusika na uhalifu na matumizi ya mihadarati ambapo kufikia sasa zaidi ya wanachama 200 wamesajiliwa.

Matokeo yake yamekuwa vijana waliokuwa wametawaliwa na matumizi ya mihadarati na uhalifu wakibadili mienendo yao, huku wakijiundia nafasi za kazi.

“Wakazi wanatoa ada ya kuegesha magari, vile vile ya kudumisha usalama, kumaanisha kwamba vijana wanaojishughulisha na kazi hii wanapokea malipo,” aeleza Bi Naliaka.

Na hivyo, viwango vya uhalifu mtaani humu vimepungua mbali na sura ya sehemu hii ambayo imekuwa ikigonga vichwa vya habari kutokana na sababu mbaya, ikibadili picha na mwonekano wake kamili.

“Kikundi hiki kimesaidia kuhepusha vijana hawa kutokana na uhalifu na maovu mengine, kwani sasa wengi wana kazi ya kufanya, na hivyo hawana muda wa ziada. Hii imeimarisha viwango vya usalama. Kwa upande mwingine, mandhari ya sehemu tofauti katika mtaa huu yamebadilika na kuwa maridadi,” aongeza.

Ni safari ambayo walianzisha Novemba mwaka jana baada ya kuona haja ya kuthibisha shughuli ya vikundi vidogo vilivyokuwa vimeanzishwa na vijana mtaani humu, kwa minajili ya kukabili visa vya uhalifu na idadi ya vijana waliokuwa wametawaliwa na matumizi ya mihadarati.

Bw Samuel Omare, Afisa mkuu mtendaji wa Transform Kayole Youth Group, akiwa katika mojawapo ya vikao na wanachama mtaani Kayole, Nairobi. Picha/ HISANI

“Awali vijana kutoka mtaa huu walikuwa wameunda vikundi vidogo katika harakati za kujitahidi kubadilisha jamii. Lakini hawakuwa na jinsi ya kudumisha vikundi hivi kwani hawakuwa na ushirika, na hivyo tukaamua kuingilia kati na kuvileta vyote pamoja,” aeleza Bi Naliaka.

Ni hapa ndipo waliamua kuanzisha kikundi kikuu, ambacho kingejumuisha makundi haya mengine kutoka mtaa wa Kayole.

Aidha, ari yao ilitokana na kwamba sehemu nyingi za mtaa huu zilikuwa zimegeuzwa na kuwa majaa ya taka, suala lililosababisha uvundo katika kila pembe ya sehemu hii.

Lakini haimaanishi kwamba hawajakumbana na changamoto huku ukosefu wa rasilimali na ala za matumizi kama vile reki, sepeto na matoroli miongoni mwa zingine, ukiwakosesha usingizi.

“Tunalazimika kukodisha ala hizi kila mara na ni ghali kwetu. Pia hatuna ufadhili ambapo mara kwa mara tunakosa cha kuwalipa vijana waliojitolea, suala linalowaweka katika hatari ya kurejelea tabia yao ya awali,” aeleza.

Lakini kulingana nao, matatizo haya kamwe hayawezi sitisha jitihada zao za kubadilisha sura na jina la mtaa wa Kayole.

You can share this post!

Kiwanda cha pamba chaiomba serikali kununua bidhaa zake

Historia ndoa kudumu dakika 3 pekee!

adminleo