• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Manusura akejeli Trump kwa kuzembea kudhibiti umiliki wa bunduki

Manusura akejeli Trump kwa kuzembea kudhibiti umiliki wa bunduki

Na MASHIRIKA

MANUSURA wa shambulio katika shule ya Parkland, Jumamosi alimlaumu Rais Donald Trump kwa kuwa na uhusiano na chama cha taifa cha bunduki (NRA) huku maelfu ya watu wakikusanyika Florida kushinikiza hatua za haraka zichukuliwe kudhibiti umiliki wa silaha.

Siku tatu baada ya mvulana aliyekuwa na bunduki kufyatua risasi na kuua watu 17 katika shule ya upili ya Marjory Stoneman Douglas, Emma Gonzalez 18, alitoa hotuba kwa wanafunzi, wazazi na wakazi wa mtaa ulio karibu wa Ft. Lauderdale.

“Kwa kila mwanasiasa anayepokea michango kutoka kwa NRA, aibu kwako!” alisema mwanafunzi huyo na kumshtumu Trump kwa kupokea mamilioni ya pesa kutoka kwa chama hicho kufadhili kampeni yake ya uchaguzi. Umati ulijibu kwa kusema : “Aibu kwake!”

“Haya yatakuwa mauaji ya mwisho ya kufyatuliwa risasi. Tutabadilisha sheria,” aliapa na kumshutumu Nikolas Cruz 19 ambaye alinunua bunduki halali licha ya kujulikana kwamba alikuwa na tabia ya kuzua ghasia.

“Suala la iwapo watu wanafaa kuruhusiwa kumiliki silaha si suala la kisiasa. Ni suala la uhai na kifo na linapaswa kukoma kuwa suala la kisiasa,” alisema Gonzalez.

Jijini Washington, wanasiasa walisema kwamba NRA halitaguswa huku Trump mwenyewe akisema sababu ya watu kuwamiminia risasi wengine linahusu matatizo ya akili bila kuzungumzia suala la kuthibiti umiliki wa silaha.

“Ikiwa rais anataka kuja na kuniambia ana kwa ana kwamba huu ulikuwa mkasa mbaya na kwamba hakuna hatua zitakazochukuliwa, basi nitafurahia kumuuliza ni pesa gapi alizopata kutoka kwa NRA,” alisema Gonzalez kwenye hotuba yake.

 

You can share this post!

Waziri wa Ulinzi Ethiopia akana tetesi jeshi limetwaa...

Paul Put ajiuzulu Harambee Stars, Okumbi achukua nafasi...

adminleo