• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Furaha kwa Awiti na wafuasi wake mahakama kuamuru alibwaga wapinzani

Furaha kwa Awiti na wafuasi wake mahakama kuamuru alibwaga wapinzani

Na RICHARD MUNGUTI

USHINDI wa Gavana wa Homa Bay Cyprian Awiti ulithibitishwa na Mahakama ya Juu Alhamisi ilipotupilia mbali maamuzi ya Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu zilizoharamisha ushindi wake mara mbili.

Jaji Mkuu (CJ) David Maraga na majaji wengine watano wa Mahakama ya Juu walisema Bw Awiti aliachaguliwa kwa mujibu wa sheria na kwamba aliwashinda wapinzani wake kwa wingi wa kura.

Katika uamuzi uliosomwa na Jaji Jackton Ojwang, mahakama hiyo ilisema Bw Awiti alimshinda Bw Joseph Oyugi Magwanga kwa kura zaidi ya 21,000.

Jaji Jackton Ojwang aliposoma uamuzi. Picha/ Richard Munguti

“Hii mahakama inatupilia mbali maamuzi ya mahakama ya rufaa na kuu kisha kuamuru Bw Awiti kuwa Gavana wa Homa Bay kama alivyotangazwa baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017,” alisema Jaji Ojwang na wenzake.

Majaji hao walibatilisha maamuzi ya Majaji Philip Waki, Otieno Odek na Fatuma Sichale wa Mahakama ya Rufaa na uamuzi wa Jaji Joseph Ngugi wa Mahakama kuu waliosema “Bw Awiti alivuruga sheria za uchaguzi ndipo ashinde uchaguzi huo mkuu.”

Jaji Maraga, Mohammed Ibrahim, Ojwang, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u na Isaac Lenaola walisema Jaji Ngugi hakufuata sheria alipokosa kuzingatia ripoti ya naibu wa msajili wa mahakama kuu aliyekagua na kuhesabu tena kura zilizopigwa.

“Majaji wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama kuu wote walipotoka kisheria walipokosa kuzingatia ripoti ya naibu wa msajili wa mahakama kuu ambaye alisema hakuona makosa yoyote aliporejelea hoja ya kuhesabu kura tena na kugagua hati za uchaguzi,” walisema Majaji hao wa Mahakama ya Juu katika uamuzi waliotoa jana alasiri.

Wafuasi walikita kambi katika lango la Mahakama ya Juu wakisubiri uamuzi. Picha/ Richard Maosi

Majaji hao walisema Jaji Ngugi alipotoka kisheria na kimaadili alipokataa kujadilia suala ya kuhesabiwa kwa kura tena ikizingatiwa ni yeye aliyekuwa ameamuru zoezi hilo lisamamiwe na naibu wa msajili wa mahakama kuu.

“Kuhesabiwa tena kwa kura na ukaguzi wa hati zilizotumika wakati wa uchaguzi ndio kigezo cha pekee mahakama hutumia kupima ikiwa uchaguzi uliendelezwa kwa mujibu wa sheria,” walisema majaji hao wa mahakama ya rufaa.

Waliendelea kusema kutozingatiwa kwa matokeo ya ukaguzi huo ulioamriwa na Jaji Ngugi ulibomoa kabisa uamuzi uliofikiwa kwamba ushindi wa Bw Awiti ulikuwa na dosari.

Majaji hao pia waliwakosoa majaji wa mahakamaya rufaa kwa kuchambua matokeo ya uchaguzi huo kama ulivyochambuliwa na naibu wa msajili wa mahakama.

Ushindi wa Bw Awiti ulikuwa umepingwa na mpinzani wake Bw Magwanga aliyedai tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ilishirikiana na Gavana huyo kughushi ushindi kwa kuiba kura.

Mawakili waliowakilisha pande zote mbili wasimama kutoa heshima zao kwa mahakama. Picha/ Richard Munguti

Bw Magwanga alikuwa amedai IEBC haikuzingatia sheria kwa kuruhusu maafisa wake kumsaidia Bw Awiti kutenda uhalifu.

Bw Magwanga aliomba kura zihesabiwe tena katika vituo 91 na hati zote zilizotumika zikaguliwe na matokeo kuangaziwa na mahakama kuu kisha atangazwe mshindi wa kiti hicho.

“Ni jambo la kushangaza Jaji Ngugi hakuzugumzia kuhusu kuhesabiwa tena kwa kura na naibu wa msajili wa mahakama licha ya kuamuru zoezi hilo litekelezwe,” walisema majaji hao wa mahakama ya upeo.

Walitupilia mbali malalamishi yote ya Bw Magwanga aliyeshindwa na Bw Awiti katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8,2017.

Bw Awiti alizoa kura zaidi ya 189,000.

Jaji Ngugi alisema IEBC haikuwasilisha fomu ilizotumia kujaza matokeo ya uchaguzi.

Naibu wa Gavana Bw Hamilton Obata alitoa wito kwa wapinzani wao washirikiane kuendeleza Kaunti ya Homa Bay.

Wafuasi wa Bw Awiti walicheza na kuimba katika mahakama ya juu baada ya ushindi wake kuthibitishwa.

You can share this post!

KERICHO: Shule ya chekechea ilivyogeuzwa danguro

Raila aachwa mpweke wenzake wakipata mamlaka

adminleo