• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
RASHID SAKA: Mpanguaji wa mikwaju motomoto anayepania kuinyakia Chelsea

RASHID SAKA: Mpanguaji wa mikwaju motomoto anayepania kuinyakia Chelsea

Na SAMMY WAWERU

MSEMO kwamba samaki mkunje angali mbichi unawiana na maisha ya ugolikipa ya mvulana Rashid Saka kutoka mtaa wa Githurai, Nairobi.

Licha ya umri wake mdogo, kipaji chake katika kandanda cha kudaka mpira kimetambulika na wengi. Saka 9, anaendelea kunolewa makali ya ugolikipa, na akijaliwa huenda akawa mmoja wa makipa ‘nyani’ humu nchini katika siku za usoni.

Mikwaju motomoto ya mastraika wenye umri sawa na wake haimbabaishi, kwa sababu ya ustahimilivu anaoonekana kuwa nao na maandalizi yake kabambe tangu akiwa na miaka 7 pekee. Kutokana na mapenzi yake katika kabumbu yanayomtia motisha, ipo siku atakuwa mnyakaji mtajika.

Mvulana huyu ndiye kipa wa timu ya shule ya msingi ya kibinafsi ya Golden Gate Academy, Nairobi, ya wachezaji kandanda walio chini ya miaka 10. Pia, staa huyu huchezea timu ya wavulana ya Githurai United wanasoka walio chini ya miaka 12, kama golikipa.

Talanta ya chipukizi huyu ilitambulika mwaka wa 2016. Angetazama mechi iliyosakatwa ikipeperushwa kwenye runinga, angeacha alichofanya almuradi alishe macho.

“Sikutaka kupitwa na habari za michezo, hasa mechi yoyote ile ya kandanda inayopeperushwa moja kwa moja kwenye televisheni na hata marudio yake wakati wa usomaji wa taarifa,” anaeleza Saka.

Ni muhimu kutaja mvulana huyu wa darasa la pili ameshawishi wazazi wake kupenda soka. Kaka yake mkubwa ni mraibu na mchezaji wa soka, na kila aliposhiriki mechi Saka hangeachwa nyuma. Alifuatilia mchuano kuanzia mwanzo hadi ulipokamilika, mvuto wake ukiwa golikipa anavyodaka mpira.

Kwa ajili ya ukakamavu wa chipukizi huyu, kocha wake Fredrick Ochieng anasema afikishapo umri wa miaka 18 atakuwa ametosha unga kudakia timu za kitaifa kama Harambee Stars na Gor Mahia.

“Anachohitaji kabla afikishe umri huo ni kumnoa mambo kadha wa kadha, hususan jinsi ya kudaka mikwaju na kuelewa siri kiasi za ugolikipa,” anaeleza.

Peter Nzuki anayechezea timu ya Tusker na Francis Kahata wa Gor Maria, walipitia mikononi mwa Bw Ochieng kuwanoa makali ya kusakata kabumbu. Yeye ndiye kocha wa Githurai United na All Stars Githurai, timu ambazo zilinoa mastaa hao.

“Sawa na nilivyowachukua wakiwa wachanga, Saka ameonesha juhudi za kuibuka golikipa bora,” akasema wakati alipohojiwa na Taifa Leo Dijitali.

Rashid Saka, golikipa chipukizi wa miaka 9 kutoka Githurai anayeamini ipo siku atapangua mashuti motomoto uwanjani Stamford Bridge, London, Uingereza. Picha/ Sammy Waweru

“Githurai United ina timu za wachezaji waliogawanywa kwa umri; chini ya miaka 10, 12, 14, 16 na walio zaidi ya 18. “Wachezaji wote ninaowapa mafunzo sharti wapitie viwango hivyo.”

Hakuna safari isiyokosa changamoto, ukosefu wa ufadhili kufanikisha juhudi zake ndio kikwazo kikuu. Ili kupata jezi na viatu vya kuchezea soka, wachezaji wenyewe ndio huchanga ili kununua.

“Uga ninaowafanyisha mazoezi umesheheni vumbi, haswa wakati wa jua kali. Hili hutuhangaisha sana, hatari kuu ikiwa magonjwa yanayosababishwa na vumbi,” anasema Bw Ochieng.

Saka hufanya mazoezi kila jioni baada ya shule, wakati wa likizo akiyatengea muda wa kuanzia adhuhuri. Ili kufikia daraja la mastaa kama Nzuki (Tusker) na Francis Kahata (Gor Mahia), Michael Kwena ambaye ni mtangazaji na mchanganuzi wa masuala ya kandanda anasema chipukizi huyu anahitaji kutambulishwa kwa vilabu tajika nchini.

Bw Kwena anasema kuna vipaji wengi ambao hawajatambulika kwa sababu ya makocha kutowajuza kwa timu zenye ushawishi na zinazoangaziwa sana na vyombo vya habari.

“Gor Mahia ni timu ya kitaifa ambayo Saka akitambulishwa kwayo atafanikiwa kustawisha talanta yake. Harambee Stars inakuza chipukizi wa kandanda kwa viwango vya umri, kocha wake afanye juhudi kumuingiza kwa timu kama hii,” ashauri.

Mdau huyu anahimiza mashirika yanayojitolea kufadhili michezo nchini yaanzishe mpango wa kulenga vipaji chipukizi hasa walio chini ya miaka 16.

“Itakuwa rahisi kuwatambua na kuwapalilia kwa sababu baadhi yao wanatoka katika familia zisizo na uwezo kifedha kuwanunulia sare na viatu,” asisitiza, akiongeza kusema kwamba wizara ya michezo na wadau husika wafanye hamasisho la kutosha kuafikia hili.

Si tu viapaji wa soka pekee, kuna waliojaliiwa talanta ya uanariadha, raga, netiboli, tenisi na michezo mingineyo wanaohitaji kupigwa jeki. Aidha, Saka ni wembe katika masomo.

“Mbali na kumnoa soka, hufuatilia wachezaji chipukizi wanavyofanya kimasomo. Nidhamu ndiyo kigezo muhimu ninachotilia maanani, siwaruhusu kuonekana kwenye baa, maeneo ya burudani, kwa sababu huko ndiko chanzo cha kushiriki maovu,” anadokeza kocha Ochieng. Anasema hushirikiana kwa karibu na wazazi wa kila mchezaji anayesajiliwa kujiunga na Githurai United na All Stars Githurai.

Saka anaienzi klabu ya Gor Mahia katika orodha ya timu zinazoshiriki KPL na Chelsea kwa timu za EPL, magolikipa wa timu hizo wakiwa ‘kipenzi’ chake. Anasema matamanio yake ni kudakia mpira timu hizo siku za usoni.

You can share this post!

Mmiliki wa kiwanda cha pombe haramu Thika aingia mitini

Mahakama yaikabidhi kampuni ya Njenga Karume shamba la...

adminleo