• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Airtel na Telkom zaungana kuzima ukiritimba wa Safaricom

Airtel na Telkom zaungana kuzima ukiritimba wa Safaricom

Na BENSON MATHEKA

KAMPUNI za Airtel Kenya na Telkom Kenya Ijumaa ziliungana ili kuimarisha hudumua zao za mawasiliano ya simu, data na kutuma pesa kwa simu nchini.

Hatua hii inalenga kukabili ushindani mkali kutoka kwa kampuni ya Safaricom ambayo ina wateja wengi nchini walioifanya kuwa na ukiritimba katika sekta ya mawasiliano.

Taarifa kutoka makao makuu ya Bharti Airtel Limited nchini India, inayomiliki Airtel Kenya ilisema kwamba kampuni hizo mbili zimekubaliana kuungana ili kuunda kampuni moja itakayotoa huduma bora kwa wateja.

“Bharti Airtel Limited, inatangaza kuwa imetia sahihi mkataba kati ya kampuni yake Airtel Networks Kenya Limited (“Airtel Kenya”) na Telkom Kenya Limited (“Telkom Kenya”) wa kuunganisha biashara zao za simu nchini Kenya kuhudumu kama ‘Airtel-Telkom’,” ilisema taarifa iliyotolewa Ijumaa.

Hata hivyo, taarifa iliongeza kuwa mkataba huo utakamilika kampuni hizi zikipatiwa idhini na idara zinazohusika za serikali ya Kenya.

Katika mkataba huo, kampuni zote mbili zilikubaliana kuunganisha biashara na shughuli zao nchini Kenya ili kubuni kampuni moja kubwa yenye uwezo wa kutoa huduma bora zaidi.

“Kampuni hiyo itawekeza katika mifumo ya kuharakisha kuzinduliwa kwa tekinolojia ili kuvutia wateja zaidi,” ilisema taarifa ya Airtel Kenya. Kulingana na kampuni hizo, kuungana kwao kutazifanya kuwa na nguvu ya kutoa huduma za mtandao kwa mashirika makubwa pamoja na biashara ndogo ndogo na zinazoendelea kustawi.

Telkom Kenya ilithibitisha kuwa ilitia mkataba wa kuungana na Airtel Kenya na kuhakikishia wateja wake kwamba watanufaika zaidi.

“Ubora wa huduma hautaathiriwa, wateja watapata thamani zaidi kutoka kwa kampuni yenye nguvu na mtandao bora zaidi na wenye nguvu pia,” Telkom ilieleza. Airtel Kenya ni kampuni ya pili kubwa ya huduma za simu Kenya baada ya Safaricom.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Kenya mwaka jana ilionyesha kuwa ilikuwa imeimarika kwa asilimia 2.5 na kufikia asilimia 19.7 ikiwa na wateja wa simu 8.7 milioni. Ripoti ilionyesha kuwa Safaricom ilipoteza asilimia 2.1 kutoka asilimia 69.1 hadi 67..

Telkom Kenya pia ilipoteza asilimia 1.3 kutoka asilimia 9 hadi 8.6. Kulingana na ripoti hiyo, Safaricom ilipoteza wateja 6,011 nayo Telkom Kenya ilipoteza asilimia 55,563 ya wateja.

CA ilisema Airtel ilipata wateja wapya 1.3 milioni kufikia mwaka jana. Itakuwa mara ya nne tangu huduma za simu zianzishwa kwa kampuni Airtel kubadilisha jina na mara mbili kwa Telkom.

Airtel ilianza kuhudumu Kenya ikijulikana kama Kencel kabla ya kubadilisha jina kuwa Celtel Kenya na kisha Zain na sasa Airtel Kenya iliponunuliwa na Bharti Airtel ya India.

Telkom Kenya ilianza huduma za simu za mkono ikijulikana kama Orange Telkom kabla ya kubadilisha jina kuwa Telkom Kenya.

You can share this post!

VIVIAN WANJIKU: Analenga kumpiku staa Priscilla Shirer...

Kipusa atambua vya sponsa vina masharti

adminleo