• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Wapinga kufukuliwa makaburi ya jamaa zao kupisha ujenzi wa daraja

Wapinga kufukuliwa makaburi ya jamaa zao kupisha ujenzi wa daraja

Na HAMISI NGOWA

PINGAMIZI kuhusu ujenzi wa mradi wa daraja linalojulikana kama Mombasa Gate Bridge katika eneo la Likoni zimeanza kujitokeza baada ya kundi la wazee kutoka eneo hilo kupinga mpango wa serikali wa kufukua makaburi ya Makame katika eneo la Peleleza.

Mwishoni mwa wiki familia kadhaa zinazodai kuzika wapendwa wao katika eneo ambalo daraja hilo litapitia, zilisema hazitakubali kufukuliwa kwa wapendwao wao zikidai hiyo ni kinyume na mila na desturi za Kimijikenda.

Msemaji wa familia hizo Bw Hamisi Mangi alidai hatua ya kuzifukua maiti zilizozikwa eneo hilo italetea familia pamoja na jamii nzima ya eneo hilo madhara makubwa.

“Tunapinga kabisa hatua ya serikali ya kufukua makaburi ya wapendwa wetu. Mimi mwenyewe Baba yangu mzazi pamoja na jamaa wangu wengine wa familia walizikwa hapa. Kutuambia makaburi yafukuliwe hiyo itakuwa kuwakosea heshima waliotangulia mbele za haki,’’ akasema.

Badala yake Bw Mangi alitaka kipande hicho cha ardhi ya ekari mbili ambayo imekuwa ikitumiwa na jamii kama sehemu yao ya kuzikana, kiweze kuhifadhiwa kwa kuzunguushiwa ukuta.

Mangi alililaumu Shirika la makavazi ya kitaifa kwa kujaribu kuzishawishi familia zilizozika wapendwa wao eneo hilo zikubali makaburi hayo kufukuliwa.

Alisema shirika hilo ndilo linafaa kuwa katika mstari wa mbele katika kutetea kuhifadhiwa kwa makaburi hayo baadhi yako na zaidi ya miaka mia moja.

MWathirwa mwengine Bw Salim Ali Kinyezi alisema kando na makaburi, eneo hilo pia liko na mapango na mizimu ambayo huenda ikaleta madhara makubwa ikiwa itasumbuliwa.

“Kuna mapango ambayo wazee wetu walitumia kwa ibada zao za kijadi na ikiwa yatasumbuliwa kuna hatari ya matatizo makubwa kujitokeza,’’ akasisitiza.

Alisema ikiwa itakuwa lazima kuyahamisha basi serikali inafaa kutoa ardhi mbadala ya kuzika mabaki ya wapendwa wao pamoja na kutoa fidia ya kati ya Shilingi 400,000 kwa kila kaburi moja akitaja kuwa eneo hilo liko na zaidi ya makaburi 1800.

Familia hizo zenye watu wao waliozikwa katika kinde hicho cha ardhi zilitoa pingamizi hizo siku chache tu baada ya afisa mmoja kutoka Shirika la turathi za kitaifa,Kenya Nationl Museum kuzuru eneo hilo walilozika wapendwa wao katika makaburi hayohuku ikiwataka kutoa makadirio ya gharama za ununuzi wa vifaa vinavyohitajika ili kuzika upya mabaki ya miili hiyo wakati itakapofukuliwa.

“Kutuambia kwamba tufanye makadirio ya gharama za kuzika upya mabaki ya miili ya wapendwa wetu tunaona hiyo ni kama kejeli,kwa sababu hawajatuambia pia ni wapi miili hiyo itazikwa baada ya kufukuliwa,’’ akasema.

Familia hizo wakiwemo waume na wake ambao walikuwa wamekusanyika katika eneo hilo la makaburi,zilifanya maombi maalum ambayo walidai ilikuwa njia ya kuwalisha tatizo hilo.

Walisema Shirika hilo liliwapa muda wa siku 10 kuanzia Jumanne ya wiki iliyopita kufana maamuzi dhidi ya suala hilo.

Serikali iko na mpango wa kujenga daraja la Mombasa Gate litakalounganisha kisiwa cha Mombasa na eneo la Pwani kusini kama njia ya kurahisishwa huduma za usafiri.

Mradi huo utafadhiliwa na serikali ya Kenya pamoja na serikali ya Japani JICA kwa gharama ya kima cha Sh82 bilioni ikiwemo fidia.

Daraja hilo litaanzia gereza la King’orani (Jela Baridi) kupitia barabara ya Lumumba hadi kituo cha zamani cha Reli hadi Likoni na kuelekea eneo la Ziwani ambako itakutana na barabara ya Dongo Kundu.

  • Tags

You can share this post!

Huenda shule 50 zikafungwa kutokana na ukame

Nyumba za wakazi 3,000 hatarini kusombwa na Bahari Hindi

adminleo