• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
Siwezi kuwaongezea wauguzi mishahara, watosheke na Sh100,000 – Gavana Ojaamong

Siwezi kuwaongezea wauguzi mishahara, watosheke na Sh100,000 – Gavana Ojaamong

Na GAITANO PESSA

GAVANA wa Kaunti ya Busia Sospeter Ojaamong amesema kuwa serikali yake kamwe haitawalipa wauguzi marupurupu yao ya huduma, ambayo yatawapandishia mishahara. 

Mwaka 2018, wahudumu hao walitia saini mkataba na serikali za kaunti ili kupokea marupurupu hayo maarufu.

Lakini katika mazungumzo na wanahabari Jumapili, Gavana Ojaamong badala yake aliwahimiza wauguzi kutosheka na mshahara wanaopata kwa sasa.

Alisema wahudumu hao tayari wanapokea mshahara mnono wa Sh100,000 ikilinganishwa na wenzao katika taaluma nyingine kama vile walimu (Sh18,000) na kuwataka kutupilia mbali mipango ya kugoma kuanzia Februari 18 mwezi huu.

“Tusiweke fikra zetu kwa mishahara pekee. Tunafaa kuhakikisha kuwa tunaboresha huduma ya afya kwa wakazi zikizidi kuathirika,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi (KNUN) tawi la Busia Isaiah Omondi. Amesisitiza kuwa wauguzi wa Busia watajiunga na wenzao katika mgomo wa kitaifa iwapo serikali ya kaunti ya Busia haitatimiza matakwa yao. Picha/ Gaitano Pessa

Aidha Bw Ojaamong aliongeza kuwa serikali yake haijapokea idhini kutoka kwa Tume ya Mishahara ya Wafanyakazi wa Serikali (SRC) kuwalipa wahudumu hao.

Matamshi ya bwana Ojaamong yanakinzana na yale ya Afisa Mkuu wa Afya Dkt Isaac Omeri aliyesema juma lililopita kuwa serikali tayari ilikuwa imetenga Sh 21m kufanikisha malipo hayo.

Tayari mwenyekiti wa chama cha wauguzi tawi la Busia (KNUN) Isaiah Omondi amesisitiza kuwa wataungana na wenzao katika kaunti za West Pokot, Kisumu, Taita Taveta, Trans Nzoia, Elgeyo Marakwet, Wajir, Mandera, Vihiga, Tharaka Nithi, Nyandarua, Nyeri, Garrissa, Samburu, Kirinyaga na Embu kugoma kuanzia Februari 18 iwapo serikali za kaunti hazitatimiza matakwa yao.

“Maswala ni mawili hapa. Watimize matakwa yetu ama tutagoma kwa sababu walikuwa na miaka miwili ya kutekeleza marupurupu haya,” amesema bw Omondi.

Wauguzi wanadai marupurupu ya Sh15,000 ya sare kila mwaka na vilevile marupurupu ya huduma ya Sh23,000 katika mwaka wa kifedha wa 2018/19.

You can share this post!

Uhuru awatuza waliobwagwa uchaguzini

Wanaopinga uongozi wa askofu AIPCA waombwa kujiengua

adminleo