• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Valentino kuadhimishwa kwa utoaji wa damu

Valentino kuadhimishwa kwa utoaji wa damu

Na Aggrey Omboki

KINARA wa Shirika la Huduma ya Kitaifa ya Utoaji Damu (KNBTS), Dkt Jospehine Githaiga ametoa wito kwa Wakenya waonyeshe upendo wa kweli kwa kutoa damu siku ya Valentine hapo Alhamisi.

Mwaka huu utoaji wa damu kitaifa wenye kauli mbiu “Onyesha Upendo” utafanywa nje ya jengo la kumbukumbu za kitaifa.

Akizungumza Jumatatu jijini Nairobi, Dkt Githaiga alisema ni asilimia moja pekee ya Wakenya ambao hutoa damu kila mara.

“Kundi linalotoa damu sana ni wale walio na umri kati ya 18 na 20. Wengi wao wako katika shule za sekondari, vyuo vikuu, taasisi na maafisa wa usalama,” alisema Dkt Githaiga.

Ili mtu kutoa damu, anatakiwa kuwa na uzani wa kilo 50 au zaidi na umri wa miaka 16 na zaidi na mwenye afya nzuri.

KNBTS iko na vituo 24 vya kutoa damu kote nchini ambavyo jukumu lake kuu ni kupokea damu kutoka kwa wahisani ambao hawalipwi chochote kwa zoezi hilo

“Vituo hivi viko Nairobi, Embu, Nakuru, Eldoret, Kisumu na Mombasa, Machakos, Kisii, Voi, Meru, Naivasha, Kakamega, Kericho, Nyeri, Garissa, Malindi, Thika, Lodwar, Bungoma, Migori, Narok, Kitui, Nandi na Kitale,” alisema kinara huyo wa KNBTS.

Wanaofaidi sana kwa damu ni akina mama wanapojifungua, wagonjwa wa saratani, wahasiriwa wa ajali za barabarani na wagonjwa wa figo wanaosafishwa damu.

KNBTS iko na uwezo wa kuhudumia hospitali 500 kwa wakati mmoja.

Dkt Githaiga alikuwa ameandamana na watoaji damu wanaongoza nchini Alpha Sanya, ambaye ni kiongozi wa mashtaka katika Kaunti ya Nakuru aliyetoa damu mara 86 tangu 1981 na Bi Aisha Dafalla ambaye ametoa mara 62.

You can share this post!

Ushindi wapandisha Wazito hadi kileleni NSL

Uhuru ashtakiwa kwa kuteua waliotemwa uchaguzini

adminleo