• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
Polisi washindwa kueleza jinsi matamshi ya Kuria yangezua ghasia

Polisi washindwa kueleza jinsi matamshi ya Kuria yangezua ghasia

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wawili wa Polisi  wameshindwa kueleza jinsi matamshi ya mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kumhusu aliyekuwa mwaniaji kiti cha urais wa muungano wa Nasa Raila Odinga yangehujumu amani.

Inspekta Kassim Baricha alimweleza hakimu mkuu mahakama ya Milimani Francis Andayi walimtia nguvuni Bw Kuria na kumshtaki kwa vile walihofia matamshi yake dhidi ya Bw Odinga yangelihatarisha amani.

Bw Kuria amekanusha shtaka la kueneza chuki ya kikabila kwa kudai katika mkutano wa hadhara matamshi yake hayakumdunisha Bw Odinga na mkewe Aida.

Bw Baricha alisema matamshi ya Bw Kuria wakati wa kampeni za Septemba 11, 2017 yalilenga kumfedhehesha Bw Odinga na “polisi walihofia huenda yakazua uhasama mkali wa kikabila.

Hakimu alifahamishwa kuwa Bw Kuria alisema maneno ya aibu kwa Bw Odinga na mkewe alipohutubia halaiki ya watu katika eneo la Wagige.

“Baada ya maneno hayo kusambazwa katika mitandao ya kijamii polisi kutoka kitengo cha kupambana uhalifu waliamriwa wamsake Bw Kuria na kumtia nguvuni,” alisema Insp Baricha.

Mbunge huyo alikutwa katika jumba la Lenana Towers na kutiwa nguvuni na kufululizwa hadi makao makuu ya uchunguzi wa jinai (DCI).

Mshtakiwa alizuiliwa na kufunguliwa mashtaka ya kueneza chuki cha kikabila.

Mahakama ilielezwa polisi waliamriwa wamchukulie Bw Kuria hatua ya haraka kabla ya mrengo wa Nasa kumkabili mwanasiasa huyo.

Insp Baricha alisema mshtakiwa alitiwa nguvuni na kufunguliwa mashtaka mara moja na nakala ya ujumbe uliokuwa ukisambazwa katika mtandao wa You Tube kunakiliwa kutoka kwa kampuni ya Safaricom.

Mahakama ilielezwa matamshi ya Bw Kuria yalijadiliwa na kuonekana yatazorotesha amani.

“Je, wewe unaelewa lugha ya Kikuyu kwa vile matamshi ya Bw Kuria yalikuwa kwa lugha hiyo?” mawakili walimwuliza afisa huyo wa polisi.

“Hapana sielewi lugha hiyo lakini waliopokea taarifa hiyo kutoka kwa mamlaka ya mawasiliano nchini CAK wanaielewa na wakifika kortini watafafanulia korti maana ya matamshi ya Bw Kuria wataambia mahakama maana yake,” alisema Insp Baricha.

Afisa mwingine wa Polisi Amos Ongera aliambia mahakama kwamba alitumwa kumkamata Bw Kuria na afisa wa mkuu wa kitengo maalum cha polisi wa kupambana na uhalifu Bw Godfrey Mburu.

“Nilimkamata Bw Kuria na kumpeleka katika makao makuu ya uchunguzi wa jinai (DCI) na kumpeana kwa kitengo cha kupambana na uhalifu,” alisema Bw Ongera.

Shahidi huyo akiongozwa na wakili wa Serikali Bi Kajuju Kirimi alisema hakujua mashtaka aliyofunguliwa Bw Kuria.

Kesi itaendelea kusikizwa Aprili 2 na 3, 2019.

You can share this post!

ANC yalia kudhalilishwa na ODM

6 kunyongwa kwa kuua na kutupa mwili mtoni

adminleo