• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
Raila adokeza kura ya kubadilisha katiba ni mwaka huu

Raila adokeza kura ya kubadilisha katiba ni mwaka huu

Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa Upinzani Raila Odinga Alhamisi alifichua kuwa huenda kura ya maamuzi kuhusu katiba ikafanyika mwaka huu.

Bw Odinga aliwataka baadhi ya wanasiasa ambao hakuwataja kuanza kutangaza msimamo ikiwa wanaunga mkono mabadiliko ya katiba au la.

“Mwaka huu utakuwa wa mabadiliko humu nchini. Tunataka kubadili mfumo wa serikali kwa kurekebisha palipo na kasoro,” akasema Bw Odinga.

“Tunataka kubadili mfumo wa serikali. Iwapo kuna mtu yeyote ambaye hataki kwenda nasi, afahamu kwamba huyo ataachwa nyuma,” akaongeza.

Kiongozi wa ODM alikuwa akizungumza alipokutana na viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, ambao waliongozwa na mlezi wao, Bi Agnes Kagure.

Bw Odinga alizungumza siku chache baada ya Naibu wa Rais William Ruto kupinga kufanyika kwa kura ya maoni ili kuongeza viti serikalini au kubuni afisi ya waziri mkuu.

Dkt Ruto, badala yake, alipendekeza kubuniwa kwa afisi ya Kiongozi wa Upinzani atakayekosoa serikali.

Naibu wa Rais aliyekuwa akizungumza wiki iliyopita, Chatham House jijini London,Uingereza, alisema haifai kwa mwaniaji aliyeibuka katika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha urais kukosa kazi licha ya kupata idadi kubwa ya kura.

Dkt Ruto, wakati huo huo, alisema kuwa haiwezekani kufanya kura ya maamuzi, sensa na kuendesha shughuli ya kurekebisha mipaka katika kipindi cha miaka mitatu iliyosalia kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Hakuna fedha za kutosha kuendesha kura ya maamuzi, kuhesabu watu na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kurekebisha mipaka,” akasema Dkt Ruto.

Mnamo Desemba mwaka jana, Rais Uhuru Kenyatta ilidokeza kuwa huenda kukawa na kura ya maoni ili kubuni viti zaidi serikalini ili kukomesha uhasama na vurugu ambazo hushuhudiwa kila baada ya uchaguzi.

Rais Kenyatta aliyekuwa akizungumza alipozuru jiji la Kisumu tangu kufanya mwafaka wa kushirikiana na Bw Odinga mnamo Machi 9, mwaka jana, alisema mfumo wa sasa haufai kwani unatenga baadhi ya jamii serikalini.

Rais Kenyatta alidokeza kwa mara ya pili mwezi uliopita wakati wa mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Hazina ya Ustawishaji wa Vijana

Bruce Odhiambo jijini Kisumu, ambapo alisema kuna haja ya kupanua serikali ili kila Mkenya ahisi kuwakilishwa.

Bw Odinga, jana alisema kura ya maamuzi itafanyika kwa njia ya demokrasia na hakuna Mkenya atalazimishwa kuunga mkono.

“Hii ni shughuli ya kidemokrasia na hiari. Hakuna mtu atalazimishwa katika mabadiliko ya Katiba,” akasema Bw Odinga.

Wanafunzi wa chuo pia waliapa kuunga mkono mabadiliko ya katiba huku wakitaka watengewe viti maalumu bungeni na katika seneti.

You can share this post!

Maafisa wa polisi mashakani kwa kugeuza gari la serikali...

AJENDA YA CHAKULA: Serikali inavyoua kilimo nchini

adminleo