• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Nyumba aliyoagiza Rais ijengwe yapakwa rangi

Nyumba aliyoagiza Rais ijengwe yapakwa rangi

Na ERIC MATARA

SIKU moja baada ya mamake Dennis Ngaruiya, kijana aliyemtumbuiza Rais Uhuru Kenyatta na shairi la kuvutia miaka minne iliyopita kuikataa nyumba aliyojengewa kufuatia agizo la Rais, mazingira ya nyumba hiyo jana yalionekana kuboreshwa na watu wasiojulikana.

Taifa Leo jana ilipofika hapo ilipata kichaka kilichokuwa kimeizunguka nyumba hiyo iliyoko katika eneo la Murunyu, eneo bunge la Bahati, Nakuru kimefyekwa, na mazingira yake kunaonekana safi, kushiria njama ya kutaka kumfunika macho Rais, kwamba amri yake ilikuwa imetimizwa.

Kichaka kilichokuwa kimeziba njia inayoelekea kwenye nyumba hiyo, yenye vyumba viwili vya kulala, pia kilifyekwa na ua unaozunguka nyumba hiyo kufanyiwa ukarabati.

Hata hivyo, hapakuwa na dalili zozote za kuonyesha kwamba Bi Damaris Wambui Kamau, mamake Ngaruiya, ambaye anatakikana kuhamia nyumba hiyo, alikuwa ameanza kuishi humo.

Nyumba hiyo pia ina maji na stima.

Kulingana na uchunguzi wa Taifa Leo, licha ya kusemekana kwamba nyumba hiyo ni mpya, inaonekana kuchakaa na yenye nyufa zinazaoashiria kwamba ilijengwa kitambo.

Nyota ya Ngaruiya na familia yake ilionekana kuanza kung’aa Oktoba 2014 alipomtumbuiza Rais Kenyatta wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku kuu ya wanajeshi katika 3KR Barracks Lanet, Nakuru.

Baadaye Rais Kenyatta alimwamuru afisa mmoja wa Ikulu kwa jina Wanjohi na wasimamizi wengine kuhakikisha kwamba familia ya Ngaruiya imepata makazi bora.

Hata hivyo mamake Ngaruiya, ambaye ni mjane, anadai kwamba amechezewa shere na baadhi ya maafisa walioamrishwa na Rais Kenyatta kuijengea familia hiyo makazi.

You can share this post!

Sababu ya serikali kuweka mpango wa kuwapa wanafunzi kondomu

Ruto akejeliwa kupinga mabadiliko ya katiba

adminleo