• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Mihadarati: Wakenya wataka ukweli baada ya DCI kusafisha jina la Joho

Mihadarati: Wakenya wataka ukweli baada ya DCI kusafisha jina la Joho

WINNIE ATIENO na SAMUEL BAYA

HISIA mseto zimeibuka nchini dhidi ya hatua ya Mkurugenzi wa Upepelezi kusafisha jina la Gavana dhidi ya madai kuwa anasakwa na maafisa wa Interpol.

Aidha habari zilisambaa mtandaoni kwamba Interpol inamsaka Bw Joho kwa kujishughulisha na ulanguzi wa mihadarati nchini na mataifa mengine.

Shutuma hii imeandama maisha yake ya kisiasa kwa miaka mingi sana huku wanasiasa wapinzani wake wakilitumia kuchafua jina lake.

Licha ya afisa mkuu wa upelelezi Bw George Kinoti kumsafisha Bw Joho dhidi ya shutuma kwamba Interpol inamsaka, Wakenya mitandaoni wameitaka afisi ya Interpol kutoa taarifa kamili kubainisha shutuma hizo.

Jumamosi Mbunge wa Nyali, Mohamed Ali naye alidai kuwa kuna majina ya wanasiasa wa Pwani ambao wameorodheshwa Interpol ambao wanashukiwa kuhusika na ulanguzi wa dawa za kulevya. Bw Ali alisema atawataja wanasiasa hao katika bunge, lakini hakusema ni lini atapasua mbarika.

Katika mtandao wa Twitter, jeshi la gavana Joho na wanaomuunga mkono walimtaka kuwashtaki wanasiasa ambao wamemhusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya.

“Tafuta wakili mzuri zaidi wapambane na hawa wabunge wanaochafua jina lako. Tunataka kesi yako iwe funzo kwa wenye hulka hii,” alisema Bw Ken Ombogo katika mtandao wa twitter.

Lakini wanasiasa wanaomtetea Gavana Joho na wachanganuzi wa kisiasa walisema hatua ya polisi kumsafisha ni dhahiri kuwa safari yake ya kuwania urais imeanza kuzaa matunda.

Wakiongozwa na mbunge wa Likoni Mishi Mboko walisema kusafishwa na polisi kumempiga jeki azma yake ya kuwania urais mwaka wa 2022.

“Pia ameweza kuonyesha Wakenya kuwa wapinzani wake ambao wanaendelea kumharibia jina kwa propaganda hizo ni warongo tu. Lakini tulijua zilikuwa tu ni propaganda kumharibia jina, tulijua wapinzani wake hawana ushahidi” Bi Mboko alisema kwa njia ya simu.

Bi Mboko alisema vyombo vyengine vya serikali vilimsafisha Bw Joho hapo awali.

“Tutamuunga Bw Joho mkono awanie urais. Wapinzani wake sasa wajitayarishe kwa kivumbi kikali,” Bi Mboko alisisitiza.

Bi Mboko alisema Bw Joho ambaye ndiye ‘mfalme’ wa eneo la Pwani amekuwa akizunguka sehemu kadha wa kadha nchini akijishughulisha na kupatanisha Wakenya kutokana na mapatano ya amani kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire alisema ni bayana kuwa waliokuwa wanamshuku Bw Joho kwa ulanguzi wa mihadarati walikuwa wanaanza kumchafulia jina.

“Wale waliokuwa wakitangatanga wakimpigia debe naibu wa Rais William Ruto awe rais sasa wamwombe radhi Bw Joho kwa kumchafulia jina ama watakiona cha mtema kuni.”alisema.

Mhadhiri wa chuo kikuu cha Pwani, Prof Halimu Shauri alimtaka Bw Joho kuwashtaki wale wote waliomhusisha na dawa za kulevya.

You can share this post!

Ruto akejeliwa kupinga mabadiliko ya katiba

Nitakuwa pasta nikistaafu kutoka siasa 2032 – Ruto

adminleo