• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Serikali sasa yakiri deni la Sh5 trilioni ni zito zaidi kwa Kenya kulipa

Serikali sasa yakiri deni la Sh5 trilioni ni zito zaidi kwa Kenya kulipa

CHARLES MWANIKI na CHARLES WASONGA

HATIMAYE Serikali imeelezea hofu kuwa huenda Kenya ikashindwa kulipa madeni yake ya kigeni, ikisema mapato yake ni madogo wala hayawezi kuiwezesha kulipa madeni hayo.

Kulingana na hati kuhusu Mkakati wa Usimamizi wa Madeni ya Serikali (MTDMS), 2019, Waziri wa Fedha Henry Rotich anapendekeza kupunguzwa kwa ukopaji kutoka nje ili kupunguza hofu ya kushindwa kulipa madeni ya sasa.

Bw Rotich anasema kupungua kwa kiwango cha mapato ya Kenya kutoka mataifa ya nje ndiko kulikolemaza juhudi za nchi kulipa madeni yake yaliyofika Sh5.3 trilioni mwishoni mwa mwaka 2018.

Kwa hivyo, kupitia stakabadhi hiyo iliyowasilishwa bungeni mnamo Alhamisi na Kiongozi wa Wengi Aden Duale, Waziri Rotich anapendekeza kuwa katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020, mikopo ya kigeni itadhibitiwa ili isipite asilimia 38 ya mapato kutoka mataifa ya kigeni huku yale ya humu nchini yakiongezwa hadi asilimia 62.

Mbinu nyingine ambayo Hazina ya Kitaifa inapanga kutumia kupunguza mzigo wa madeni ni kutenganisha ukopaji kutoka nje na ule wa humu nchini, ili kutoathiri uwezo wa sekta ya kibinafsi kupata mikopo katika soko la kifedha.

“Tunapendekeza kudhibiti mikopo kutoka nje kuwa asilimia 38 ya mapato kutoka nje na asilimia 62 kwa mikopo kutoka humu nchini,” Bw Rotich akasema katika stakabadhi hiyo iliyowasilishwa bungeni sambamba na bajeti ya 2019/20 ya Sh2.7 trilioni.

Kufikia sasa Kenya inadaiwa Sh2.6 trilioni inazofaa ilipe upesi, kiwango ambacho ni nusu ya Sh5.3 trilioni, jumla ya pesa ambazo Kenya inadaiwa. Kupunguzwa kwa kiwango cha mikopo kutoka nje inayolipiwa riba ya juu (commercial loans) kunaashiria kuwa Waziri Rotich anapanga kuzuia mikopo kupitia hati za dhamana ya Eurobond.

Mnamo 2015 hadi 2017 mrengo wa upinzani, NASA, ulipinga mikopo hii ukidai kuwa Sh275 bilioni zilizokopwa kwa njia hii zilifujwa au kuibwa.

Serikali imejitetea kwamba imekuwa vigumu kwake kupata mikopo ya riba ya chini (concessional loans) kwa sababu Kenya inaorodheshwa kama taifa lenye mapato ya kadri. Hii ina maana kuwa Waziri Rotich anakabiliwa na chaguo moja pekee; kuendea mikopo ya riba ya juu kama vile Eurobond.

“Lakini kupanda kwa riba katika soko la kimataifa la mikopo kumepandisha gharama ya ulipaji mikopo ambayo muda wake wa kuanza kulipa umetimu, na gharama ya mikopo ya kigeni kwa ujumla,” Bw Rotich anasema katika stakabadhi hiyo.

You can share this post!

Aliyeshtakiwa kuuma mamake afunguka alikuwa anamchukia

FUNGUKA: ‘Tabia zake chwara zanisisimua ajabu’

adminleo