• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Raila na Miguna Miguna warukiana

Raila na Miguna Miguna warukiana

Na WANDERI KAMAU

Kwa ufupi:

  • Kiini cha majibizano ni madai ya Bw Miguna kwamba Dkt David Ndii na  Bw Norman Magaya wanashirikiana kisiri na Jubilee
  • Kuhusu Dkt Ndii, Bw Miguna alisema kwamba alikuwa akipinga hatua ya kumwapisha Bw Odinga
  • Bw Odinga alipuuzilia mbali madai ya B w Miguna, na kushikilia ana imani kamili na utendakazi wa Dkt Ndii na Bw Magaya
  • Wawili hao waliwahi kuwa washirika wa karibu ila wakakosana na Bw Miguna alijitokeza kumshutumu Bw Odinga kwa kuandika kitabu Peeling Back the Mask’

VITA vya maneno vilizuka Jumatatu ndani ya Muungano wa NASA baina ya kinara Raila Odinga na mwanasiasa Miguna Miguna kuhusiana na madai kuwa kuna watu wanaofanya kazi katika muungano huo ambao ni vibaraka wa Jubilee.

Kiini cha majibizano hayo ni madai ya mnamo Jumapili yaliyotolewa na Bw Miguna kwamba mwenyekiti wa Kamati Tekelezi ya NASA Dkt David Ndii na Afisa Mkuu Mtendaji wa muungano huo Bw Norman Magaya wanashirikiana kisiri na Jubilee kusambaratisha upinzani.

Bw Miguna angali nchini Canada baada ya kufurushwa nchini wiki mbili zilizopita,

Hapo Jumatatu Bw Odinga alimjibu Bw Miguna kwa taarifa akipuuzilia mbali madai yake, na kushikilia kuwa muungano huo una imani kamili na utendakazi wa Dkt Ndii na Bw Magaya.

“Tungependa kutoa hakikisho kama NASA kwamba tuna imani kamili na utendakazi wa Dkt Ndii na Bw Magaya, kwani wamejitolea kikamilifu kutetea maslahi ya muungano wetu. Madai yoyote dhidi yao ni hatari sana kwa safari na malengo tuliyo nayo,” akasema Bw Odinga.

Dkt Miguna Miguna alikuwa katika mstari wa mbele kwenye maandalizi na uapishaji wa kinara wa NASA kuwa ‘rais wa wananchi’ Januari 30, 2018. Kwa sasa, wametofautiana kisiasa. Picha/ Maktaba

Wasaliti

Muda mfupi baada ya taarifa ya Bw Odinga, Bw Miguna alijibu kwenye mtandao wa Twitter akisema anashikilia kauli yake kuwa Dkt Ndii na Bw Magaya ni wasaliti.

“Sitabadilisha msimamo wangu. Ninasisitiza kwamba Dkt Ndii na Bw Magaya ni wasaliti wakuu,” akasema wakili huyo.
Kwenye ujumbe alioweka katika mtandao mnamo Jumapili, Bw Miguna alilalamika kwamba wawili hao wamekuwa kimya tangu alipofukuzwa Kenya na kudai kuwa wanalipwa na Jubilee kusambaratisha NASA.

“Magaya anashirikiana kisiri na Jubilee. Alipokea hongo ya Sh30 milioni kuondoa kesi ambayo alikuwa amewasilisha dhidi ya Gavana Mike Sonko wa Nairobi. Hii ilikuwa kama kulipiza kisasi dhidi ya Bw Raila alipokosa kuteuliwa kama mbunge maalum katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA),” akadai Bw Miguna.

Kuhusu Dkt Ndii, Bw Miguna alisema kwamba alikuwa akipinga hatua ya kumwapisha Bw Odinga, kando na kutishia kujiondoa katika muungano huo.

 

Pigo

Hatua ya Bw Odinga kupuzilia mbali madai hayo inaonekana pigo kwa Bw Miguna, ambaye amejitokeza kama mtetezi mkuu wa Bw Odinga, hasa baada ya kumwapisha kama “rais wa wananchi” mnamo Januari 30.

Pia uamuzi wake kumjibu kiongozi huyo wa ODM hata baada ya kutoa kauli yake huenda ikakasirisha wafuasi wa kigogo huyo wa upinzani kwani inaonekana kama kumkosea heshima.

Wawili hao waliwahi kuwa washirika wa karibu wa kisiasa kwenye Serikali ya Muungano ila wakakosana vikali baadaye, ambapo Bw Miguna alijitokeza waziwazi kumshutumu Bw Odinga.

Tofauti zao zilipelekea Bw Miguna kuandika kitabu ‘Peeling Back the Mask: A Quest for Justice in Kenya’ ambacho kilimkosoa vikali Bw Odinga, hasa kuhusiana na uongozi wake alipohudumu kama Waziri Mkuu katika serikali ya muungano iliyoongozwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Bw Miguna alionekana kuchukua hatua za kurudisha uhusiano wao baada ya uchaguzi wa Agosti 8 mwaka jana alipojiunga na NASA kwa kauli kuwa Bw Odinga alikuwa ameshinda uchaguzi huo.

 

 

You can share this post!

Msamaha wa Atwoli wakosa kutuliza joto

TAHARIRI: Umma usitwikwe mzigo wa madeni

adminleo