• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Wazazi wanunulia shule basi kama zawadi ya matokeo bora

Wazazi wanunulia shule basi kama zawadi ya matokeo bora

Na DERICK LUVEGA

WAZAZI katika Kaunti ya Vihiga wamenunulia shule basi na kujenga madarasa ya mamilioni ya pesa kama zawadi ya matokeo bora kila mwaka katika mitihani ya kitaifa.

Hatua hiyo isiyo ya kawaida ilianzishwa katika mwaka wa 2015 na imepelekea wazazi walio na watoto katika shule hiyo ya umma ya St Francis, Hambale inayosimamiwa na Kanisa Katoliki kupata basi lililogharimu Sh6.5 milioni na jengo jipya la madarasa lenye orofa tatu kupitia kwa harambee.

Wazazi hao jana walikabidhi zawadi hizo kwa shule kwenye hafla iliyofanywa shuleni humo katikati mwa mji wa Mbale, Kaunti ya Vihiga.

Shule hiyo ambayo ina sehemu za malazi na kutwa imekuwa ikipata matokeo bora hasa katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE).

Mwaka uliopita, iliongoza katika Kaunti Ndogo ya Vihiga kwa kutoa alama 340 kwa wastani huku ikishindana na shule nyingine bora za eneo hilo ambazo ni Mululu, Mudasa, Serve na Shalom.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa shule hiyo, Bw Kennedy Keseko alisema wazo la kutuza shule hiyo lilitolewa na wazazi katika mwaka wa 2015.

Bw Keseko alisema wazazi walijitolea kufadhili mpango huo wao wenyewe kupitia kwa michango licha ya serikali kuzuia wazazi kutozwa fedha katika shule za umma.

“Wazazi waliamua kutuza shule hii kwa jinsi imekuwa ikiwapa watoto elimu bora na nidhamu. Hii ndiyo sababu wamekusanyika hapa kutoa zawadi hizi kama ishara ya shukurani,” akasema Bw Keseko.

Alieleza kuwa jengo hilo lina maktaba, madarasa 12 na maabara ya kutoa mafunzo ya kompyuta.

You can share this post!

Wauguzi watishia kuhama baada ya wenzao kudungwa visu Mama...

Hospitali yajitetea kuhusu mama kubeba mtoto mfu hadi...

adminleo