• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
THERESIA BHOKE: Mtangazaji, mwigizaji na mwanamuziki shupavu

THERESIA BHOKE: Mtangazaji, mwigizaji na mwanamuziki shupavu

Na JOHN KIMWERE

ANAWAHIMIZA wenzake kuwa wabunifu katika sekta ya usanii pia wajitume kwenye gemu kukomesha mtindo wa kuketi kijiwe kusubiria ajira.

Anasema ukuaji wa teknolojia duniani unatoa nafasi mwafaka kwa wenye talanta kubuni ajira badala ya kutengemea kuajiriwa.

Aidha anawahimiza kutokuwa wepesi wa kuvunjika moyo hasa mikakati yao inapokwenda mrama. Hata hivyo anasisitiza kwamba ‘mtaka cha mvunguni sharti ainame’ maana hakuna mafanikio hupatikana rahisi.

Teresia Bhoke amehitimu kama mtangazaji na mwanamitindo, mwigizaji anayeibukia sawa na mwanamuziki. Binti huyu aliyegeukia uigizaji mwaka 2018 ni mzawa wa eneo la Kuria.

”Nimepania kujituma mithili ya mchwa kudhihirishia ulimwengu kwamba eneo la Kuria wapo wanamuziki wa kike vile vile waigizaji kinyume na kasumba ya wengi,” alisema na kuongeza kuwa anafahamu wengi wanamlinganisha na kioo cha jamii ambapo wanadada wenzie wanamtazama kwa makini wakidhamiria kufuata nyayo zake.

Teresia Bhoke. Picha/ John Kimwere

Kisura huyu anayelenga kufikia levo ya kimataifa katika sekta ya muziki na uigizaji aliwahi kuchapa kazi katika runinga ya KBC miaka iliyopita.

Teresia ambaye kimuziki anajulikana kama Triza B, hughani nyimbo za kizazi kipya kwa mitindo tofauti ikiwamo Afro-pop, Chakasha na Zulka.

Mwishoni mwa 2018 aliachia fataki moja iitwayo ‘Chali’ inayozidi kupokelewa vyema na vyombo vya habari bila kuweka katika kaburi la sahau mashabiki wake.

Anasema ni teke inayowapangawisha mashabiki siyo haba. Aidha anajivunia kutoa nyimbo kadhaa: ‘Acha nideke’, ‘Nitakufa nawe,’ ‘Tulia,’ ‘Waniumiza,’ na ‘Niambie.’

Katika upande wa mwana mitindo amewahi kuingia dili ya kuhusishwa kwenye picha za matangazo ya kibishara na kampuni ya simu ya Safaricom pia kampuni moja ya unga nchini.

Katika uigizaji miaka minne iliyopita alishiriki muvi iliyokwenda kama ‘Lies that Bind’ iliyorushwa kupitia runinga ya NTV ambayo humilikiwa na Shirika la Nation Media Group.

Mwezi Desemba 2018 pia aliigiza kwa kipindi cha ‘Auntie Boss’ ambacho pia hupeperushwa kupitia NTV.

Kadhalika tangu mapema 2018 amekuwa akiigiza kipindi cha ‘House of Commotion’ ambacho hupeperushwa kupitia runinga ya KTN Burudani.

Aliposhirika katika picha ya tangazo la kampuni ya Safaricom. Picha/ John Kimwere

“Nataka kutinga levo ya kimataifa katika uigizaji vile vile natamani sana kufanya kazi na waigizaji wa bongo,’ alisema na kuongeza kwamba ni ndoto anayoamini ataitimiza ndani ya miaka michache ijayo.

Katika mpango mzima anasema kwa ushirikiano na wenzie wanapania kufanya projekti nyingi tu kupitia brandi inayofahamika kama Connie Kabarry Production inayolenga kutengeneza muvi za Afro Cinema za Kikenya.

Kampuni hiyo inalenga kupeleka kundi la Wakenya kadhaa nchini Nigeria kutengeneza muvi kadhaa wakishirikiana na wenzao katika taifa hilo.

Kwa mtazamo wa wengi hatua hiyo inatazamiwa kuleta mwamko mpya katika filamu na muvi nchini. Anasema Wakenya wanaweza kufanya vizuri zaidi sawia na wenzao katika mataifa yanayoendelea kama Nigeria, Tanzania na Afrika Kusini kati ya mengineo.

You can share this post!

ELIZABETH MARONGA: Utalia mwenyewe ukikubali kuigiza bila...

BETHA ACHIENG: Mkali wa video za kuvumisha nyimbo

adminleo