• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
TAHARIRI: HELB ipunguze faini ya mikopo

TAHARIRI: HELB ipunguze faini ya mikopo

NA MHARIRI

JUMATANO Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Vyuo (HELB) inaandaa kikao cha kutangaza mkakati wake mpya wa mwaka 2019.

Kwenye kikao hicho kitakachoandaliwa katika hoteli ya Laico Regency, Nairobi, halmashauri hiyo inatarajiwa kutangaza matokeo ya utendakazi wake wa mwaka uliokamilika mbali na kuweka wazi mpango wake wa mwaka huu na zaidi.

HELB ni shirika muhimu zaidi kwa elimu humu nchini hasa kwa sababu ndiyo iliyotwikwa jukumu la kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mikopo ya kuwawezesha kuhitimisha masomo yao ya chuo kikuu ama chuo cha wastani.

Wapo watu wengi zaidi waliofanikiwa maishani kutokana na mkopo wa HELB. Lakini pia wapo wengi zaidi, hasa baada ya serikali kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na chuo kikuu kutoka 10,000 hadi sasa karibu 90,000, ambao ama wamelazimika kukatiza masomo yao au hata kutatizika zaidi kwa kunyimwa mkopo huo.

Huku HELB ikiendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wengi maskini, wapo wanaostahili kupata mkopo huo ambao wamenyimwa huku wale wasiostahili wakipewa.

Kwa mfano, wapo wanafunzi maskini zaidi ambao baada ya kukosa padogo kupata mkopo walipouomba kwa mara ya kwanza, wameendelea kunyimwa hata katika miaka inayofuatia licha ya shirika hilo kudai kuwa kuna rufaa. Helb imefanya vigumu kwa wanaokata rufaa hiyo kupata pesa hizo.

Akili razini inafaa ielekeze wakuu wa HELB kujiuliza; iwapo wana uwezo wa kuwapa wanafunzi wa stashahada (diploma) mikopo hiyo -wanafunzi ambao hapo awali hawakuwa wakipokea -sababu gani inawanyima wengi wa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaokata rufaa ilhali wanahitaji sana fedha hizo? Sharti shirika hilo lipambanue upya kipaumbele chake katika kongamano lake la leo.

Suala muhimu la pili ni je, kwa nini HELB inawaadhibu Wakenya vikali jinsi hii? Wapo wanafunzi walionufaika kutokana na mkopo wa HELB ambao baada ya kumaliza chuo, walitatizika kupata ajira, hivyo wana uwezo mdogo wa kuanza kulipa deni hilo.

Inapochukuliwa kuwa wengi wa wanafunzi wanaoomba mkopo huo wanatoka katika familia maskini, inashangaza kuwa HELB huanza kuwapiga faini ya Sh5000 kila mwezi, baada ya mwaka mmoja wa kufuzu kwao. Swali ni je, mbona wasitoze faini ndogo?

Aidha, kwa nini hata baada ya waliodhaniwa kukwepa kulipa mkopo huo, wanapoanza kuulipa, bado wanalazimika kulipa faini hiyo nzima?

Kwa nini wasipunguziwe faini hiyo kwa kiasi kikubwa iwezekanavyo?

You can share this post!

Minara ya Kemboi, Vivian kuzinduliwa mjini Eldoret

NGILA: Tovuti za habari feki ni tisho kwa taaluma ya...

adminleo