• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
NGILA: Tovuti za habari feki ni tisho kwa taaluma ya uanahabari

NGILA: Tovuti za habari feki ni tisho kwa taaluma ya uanahabari

Na FAUSTINE NGILA

YAMKINI kila mtu anayetegemea mitandao ya kijamii kupata habari za matukio ya kila siku amekumbana na vichwa vya kuvutia kuhusu habari mbalimbali, lakini anapofungua kusoma habari zenyewe, anatamaushwa na yaliyomo.

Vichwa hivi huahidi msomaji kuwa habari mle ndani ni ya kipekee, lakini huishia kumkera msomaji kutokana na uandishi mbaya uliomo na taarifa zisizo na manufaa yoyote.

Katika enzi hizi za dijitali, inaudhi kuwaona baadhi ya wahariri wa mitandaoni wakiandika vichwa vya kiujanja ili kuvutia hadhira kubwa huku kanuni na sheria za uanahabari zikipuuzwa.

Mara nyingi taarifa zilizomo ni za uwongo, zinapotosha, zinaharibia watu sifa, zina picha za ngono huku nyingi zikiwa matangazo ya bidhaa.

Ingawa juhudi hizi zinalenga kuwaletea fedha wamiliki wa tovuti hizi, hadhira kubwa wanayopata hupungua jinsi muda unavyosonga, na hatimaye hubandikwa jina ‘tovuti za habari feki.’

Hii hutokana na wao kupuuza ya habari zinazomhusu msomaji zilizofanyiwa utafiti wa kina, na kuchapisha habari zenye porojo za kuwatega wasomaji kupitia mnato wa aina yake. Mwishowe biashara ya aina hii hatimaye huporomoka.

Mfano ni kampuni ya kimataifa inayotambulika kwa habari zenye mvuto wa juu, BuzzFeed, ambayo majuzi imelazimika kuwatimua wafanyakazi 218 ili kuinua mapato yake kwa kuchapisha ‘habari ambazo wasomaji wanapenda.’

Ilichosahau kampuni hii ni kuwa wasomaji hawapendi kuahidiwa habari kwa kina kisha kupewa habari hewa, hali sawa na kumwahidi mtoto nyama kisha kumpa mfupa.

Kinachowakasirisha wasomaji ni uwongo kwenye vichwa vya habari hizo mitandaoani, ambao huwalazimu kukosa imani na tovuti hizi.

Hapa Kenya, utazipata tovuti hizi katika mitandao yote ya kijamii zikijifanya kuwapa wasomaji habari kemkem za matukio muhimu, lakini unaposoma habari zake, utakerwa na maandishi na ujumbe uliomo.

Ingawa nakubali kuwa uwezo wa data na uchanganuzi wa hadhira umechangia pakubwa kuleta mageuzi muhimu kwa taaluma ya uanahabari, mtindo wa kuchapisha habari feki na potovu unafaa kukomeshwa.

Mwenendo huu unazidi kuua jukumu la vyombo vya habari la kuwapiga msasa viongozi wasiowajibikia kazi zao, kuwaanika wavunja sheria na kuikosoa jamii.

Umefika wakati kwa Wizara ya Habari na Mawasiliano (ICT) ikishirikiana na Baraza la Kitaifa kuhusu Uanahabari (MCK) kuanza kutekeleza sheria kuhusu habari feki, kwa kutoa onyo kwa tovuti hizi na kuzima zile zitakazokaidi sheria.

Ni tisho kuu kwa mustakabali wa uanahabari katika nchi hii iwapo serikali itazidi kuruhusu tovuti hizi zenye ‘wanahabari’ wazembe kuzidi kuweka taarifa zisizothibitishwa mitandaoni .

[email protected] 

You can share this post!

TAHARIRI: HELB ipunguze faini ya mikopo

PICHA: Mzozo wazua kubomolewa kwa nyumba 20 Railways,...

adminleo