• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
‘2022 ni zamu ya Mlima Kenya Mashariki kutwaa uongozi wa taifa hili’

‘2022 ni zamu ya Mlima Kenya Mashariki kutwaa uongozi wa taifa hili’

Na GEORGE MUNENE

Aliyekuwa waziri, Joseph Nyaga, Jumatano alijiunga na mjadala wa siasa za urithi na kuwataka wakazi wa eneo la Mlima Kenya Mashariki kuanza kuandaa mmoja wao kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atapostaafu.

Katika hatua nyingine inayoonekana kulenga kumharibia Naibu Rais William Ruto nafasi ya kuwa rais baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Nyaga alisema wakati umefika wa mwanasiasa kutoka eneo hilo kuongoza nchi hii.

Bw Nyagah alisisitiza kuwa Kaunti za Kirinyaga, Embu, Tharaka Nithi na Meru zinazounda eneo la Mlima Kenya Mashariki zina uwezo wa kumtoa rais.

“Ninawahimiza viongozi kutoka eneo hili kuzinduka na kuanza kujiandaa jinsi ya kuwa na mgombea urais mmoja kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 ili ashindane na wagombeaji wengine ambao wanamezea mate kiti hicho,” alisema Bw Nyaga akiwa kijiji cha Difathas, Mwea Mashariki Kaunti ya Kirinyaga.

Mwanasiasa hiyo aliwapa changamoto viongozi wa eneo hilo kutoogopa kuandaa mmoja wao kugombea kiti hicho.

“Nimekuwa ODM na Kanu na kwa hivyo Wakenya watakubaliana nami kwamba mimi sio mkabila lakini ninaamini kwamba rais anafaa kutoka eneo hili wakati huu,” alisema.

Alimwambia naibu spika wa seneti Bw Kindiki Kithure na Gavana wa Meru, Kiraitu Murungi pamoja na viongozi wengine kutoka eneo hilo kukoma kusema watakuwa wagombea wenza wa watu wengine.

“Tumekomaa na tunaweza kuongoza nchi hii vyema. Kwa hakika, eneo letu lina wapigakura 2 milioni na tukiungana na binamu zetu, ndugu na dada kutoka eneo la Kati na maeneo mengine ya nchi, tunaweza kushinda urais rahisi sana,” alisema Bw Nyagah.

Mwanasiasa huyo ambaye aliwahi kugombea urais alisema mtu atakayetambuliwa na kuungwa na viongozi wote wa eneo hilo anafaa kuanza kuzunguka Rift Valley, Nyanza, Magharibi, Pwani na maeneo mengine kusalimia watu na kuwaeleza azima yake ya kuwa rais.

“Viongozi wanafaa kuwa wajasiri kama mimi. Niligombea urais na niliorodheshwa wa tatu kote nchini. Sasa tuko na viongozi vijana, waliosoma na walio na nguvu kutoka eneo hili wanaoweza kugombea na kushinda urais,” alisema.

Kuhusu mjadala wa kurekebisha katiba, Bw Nyagah alisema anaunga wito huo kikamilifu akisema hatua hiyo itahakikisha makabila yote Kenya yamewakilishwa serikalini.

Alisema Wakenya wamechoshwa na mfumo wa serikali ambapo mshindi hutwaa mamlaka yote.

“Katiba ikibadilishwa, tutakuwa na mfumo wa serikali ambapo tutakuwa na waziri mkuu mwenye mamlaka makuu na manaibu wake wawili. Tutakuwa pia na rais na hii inamaanisha serikali itashirikisha wote na kuwa na uwiano Kenya.

Bw Nyagah alisema wale wanaopinga kura ya maamuzi ni maadui wa nchi na wanafaa kukataliwa na Wakenya wote.

Kuhusu vita dhidi ya ufisadi, alimpongeza Rais Uhuru Kenyatta na akamhimiza asilegeze kamba. “Rais anafanya kazi nzuri kwa kupiga vita ufisadi na iwapo vitafaulu, basi uchumi wa Kenya utastawi,” alisema na kumuomba Rais kuelekeza vita hivyo katika serikali za kaunti.

You can share this post!

Waliokaidi kulipa mikopo ya HELB kuwindwa na polisi hadi...

Vipi nitajibu mashtaka na sielewi Kiingereza? mwanafunzi...

adminleo