• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
TAHARIRI: Kila raia ana haki ya huduma za afya

TAHARIRI: Kila raia ana haki ya huduma za afya

NA MHARIRI

KISA cha mwanamume kujaribu kutorosha mwanawe hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kwa kukosa Sh56,000 za bili ya matibabu, ni dalili ya mfumo wa afya ulioshindwa kutimiza mahitaji ya kimsingi ya raia wake.

Visa sawa na hiki vimekuwa vingi lakini wengi hawavifahamu kwa kuwa havijaripotiwa kwenye vyombo vya habari huku wengine wakifanikiwa kutoroka wapendwa wao hospitali bila kulipa bili.

Hii inaonyesha hali ya kukata tamaa kimaisha miongoni mwa Wakenya wengi kiasi kuwa wanaweza kufanya lolote ili waweze kuishi angaa kwa siku moja zaidi.

Hali katika sekta ya afya imekuwa mbaya kiasi kuwa huduma bora za afya zimekuwa ni kwa wale tu walio na pesa za kulipia. Ole wako kama hauna pesa!

Serikali inapasa kukumbuka kuwa huduma bora za afya ni haki ya kimsingi kwa kila mwananchi kwa mujibu wa Katiba. Kwa kukosa kuweka mifumo bora ya huduma za afya, serikali inakikuka haki za binadamu.

Kwa sababu ya ufisadi, utepetevu, ukosefu wa maono ya ustawi wa nchi, ubinafsi, ulafi wa madaktari na kutowajali wananchi wa kawaida, mfumo wa afya nchini umekuwa sawa na ule wa kilimo ambao badala ya kuinua taifa unalitumbukiza kwenye majanga.

Kutokana na hali hii, maskini wanakufa kila uchao kutokana na magonjwa ambayo ni rahisi kutibiwa huku wengine wakitumbukia kwenye umaskini zaidi wanapolazimika kuuza kidogo walicho nacho ili kulipia gharama za matibabu.

Madaktari wengi nao wamegeuka fisi waliojaa ulafi kwa kuongozwa na tamaa ya pesa kuliko kujali maisha ya binadamu. Kwa mfano unawezaje kukosa kumpa binadamu mwenzako aliye hali mahututi huduma ya kwanza hadi alipe? Huu si utu!

Masuala haya yanadhihirisha haja ya serikali na wahusika wengine kuweka tumbo zao kando na maisha ya binadamu mbele.

Hii itawasaidia kubuni njia za kuhakikisha kile Mkenya anapata huduma bora za afya, na hivyo hakutakuwa na haja ya kutorisha watoto hospitalini kwa kushindwa kulipa bili.

Ni bora kulainisha mambo wakati kuna fursa kwa sababu tukiendelea kujikokota, kabila la maskini siku moja litafika mwisho wa kukata tamaa, na matokeo yake yanaweza kusambaratisha taifa.

You can share this post!

Kisura aponea kipigo kuuza mbuzi ya mume aponde raha

Mama asimulia mahangaiko ya bintiye aliyenajisiwa na...

adminleo