• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
Madeni yazidi kuisakama serikali

Madeni yazidi kuisakama serikali

Na BERNARDINE MUTANU

MDHIBITI wa bajeti ameonya kuhusiana na kiwango kikubwa cha deni la serikali kutokana na kuwa zaidi ya nusu ya mapato yote nchini hulipa madeni.

Kati ya Sh100 bilioni ambazo zimekusanywa na serikali Sh61 bilioni zimetumiwa kulipa madeni mwaka huu wa kifedha.

Hazina ya Fedha imekadiria kuwa Sh1.1 trilioni zitatumiwa kulipa madeni katika mwaka wa kifedha wa 2019/20 ambao unaanza Julai, au asilimia 61 ya mapato yote yanayotarajiwa ya Sh1.87 trilioni.

Kumaanisha kuwa serikali itasalia na Sh700 bilioni pekee za maendeleo katika bajeti yake.

Kulingana na mdhibiti wa bajeti, itakuwa vigumu sana kwa serikali kuhimili na kukuza maendeleo na kiwango hicho cha fedha.

Awali, Hazina ya Fedha imejitetea kwa kusema kuwa serikali ina uwezo wa kuhimili kiwango cha sasa cha deni cha Sh5.226 trilioni, ambacho ni asilimia 52.7 cha mapato yote ya serikali.

Kulingana hazina hiyo, serikali itashindwa kuhimili kiwango cha sasa cha deni ikiwa kitakuwa ni asilimia 70 ya mapato yote ya serikali.

Lakini Waziri wa Fedha Henry Rotich amependekeza kupunguzwa kwa kiwango cha mikopo ya kimataifa kwa lengo la kuirahisishia serikali kulipa deni lake.

Madeni ya kimataifa kwa sasa ni Sh2.6 trilioni, karibu nusu ya deni lote la serikali. Tayari, changamoto za kifedha nchini zinashuhudiwa, huku wauguzi wakiendelea na mgomo kutaka kulipwa kuambatana na mkataba.

You can share this post!

Ni visiki vipi vinahujumu juhudi za kumaliza ukeketaji...

Melly asafisha kozi zinazodaiwa kuwa ‘feki’

adminleo