• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
NEMA yazima waliofukua maiti kujenga soko makaburini

NEMA yazima waliofukua maiti kujenga soko makaburini

Na PETER MBURU

MAMLAKA ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) imesimamisha ujenzi wa soko la Sh1.3 milioni katika eneo ambapo palikuwa kaburi kaunti ya Taita Taveta, na kuamrisha serikali ya kaunti hiyo kufanya utafiti wa kimazingira kwanza, kabla ya kulijenga.

Soko hilo linajengwa katika kijiji cha Bura Ndogo, lakini mshirikishi wa Nema Edith Kalo akasema mamlaka hiyo iliamrisha idara ya kaunti ya biashara kuwa ujenzi usitishwe.

Bi Kalo alisema kuwa hatua zote za ujenzi hazikuzingatiwa kabla ya ujenzi kuanza.

“Sharti wadokeze kuwa wanataka kubadilisha kaburi hilo kuwa soko na wajumuishe ripoti za ukaguzi na ya athari za kijamii na kitamaduni,” akasema.

Aidha, afisa huyo wa Nema walieleza kuwa sharti serikali iseme kuwa itatupa sehemu za maiti ambazo zitatolewa ndani ya ardhi, ambazo zitafukuliwa wakati wa ujenzi.

Alisema kuwa endapo maafisa wa kaunti hawatashughulikia mambo hayo, mamlaka hiyo itatafuta amri ya korti kusimamisha ujenzi wa mradi huo.

Matukio haya yaliibuka baada ya wakazi kulalamika kuwa mwanakandarasi anayeendesha ujenzi wa soko hilo ameanza kufukua maiti za wapendwa wao, ili kujenga soko.

Kaburi la Bura Ndogo lilijaa zaidi ya miaka 30 iliyopita, ndipo ardhi nyingine ikatengwa kuwa mahali pa watu kuzikwa.

Wakazi wa eneo hilo sasa wanasema kuwa kutokana na hali ya soko hilo kujengwa juu ya kaburi, huenda matukio mabaya yakaanza kukumba mradi huo ama eneo hilo kwa jumla.

“Tunaweza kukumbwa na janga kwa kuwasumbua wafu. Hakuna yeyote aliye tayari kufanyia biashara hapo kwani haitaendelea,” akasema Bw Barnabas Maimbo, mkazi.

Lakini waziri wa ardhi kaunti hiyo Getrude Shuwe alisema kuwa ni wakazi waliopendekeza kuwa soko hilo lijengwe katika ardhi hiyo.

“Hawana mahali mahususi pa kufanyia biashara, hivyo wakazi walipendekeza eneo hilo. Serikali ya kaunti inatekeleza kile kilipitishwa na wakazi,” akasema Bi Shuwe, akiahidi kuwa sehemu za maiti zinazofukuliwa zitazikwa mahali pengine.

Diwani wa Bomeni alisema kuwa ujenzi utaendelea, lakini akasema kwa maiti zinazofukuliwa, hafla ya utakazaji itafanywa, kisha zizikwe mahali pengine.

“Tutachinja mbuzi hapo ili kufukuza hatari yoyote kabla ya kuzika tena maiti hiyo,” akasema.

You can share this post!

Ng’eno bingwa wa Safi Half Marathon Morocco

Kutumia simu ukila kutakunenepesha – Utafiti

adminleo