• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Abagusii kuteua wa kuunga mkono kati ya Ruto na Matiang’i

Abagusii kuteua wa kuunga mkono kati ya Ruto na Matiang’i

Na RUTH MBULA

VIONGOZI kutoka eneo la Gusii wamejipata katika njia panda kuhusu ni nani kati ya Naibu wa Rais, Dkt William Ruto na Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i wanayepasa kujihusisha naye hadharani.

Hali hii imejiri baada ya Dkt Matiang’i kupandishwa cheo na Rais Uhuru Kenyatta kusimamia utekelezaji na ushirikishi wa miradi ya serikali.

Baadhi ya wadadisi wanasema hatua hiyo imeathiri juhudi za Dkt Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi wa 2022.

Kuna baadhi ya viongozi wanahisi kwamba jamii hiyo sasa ina mwana wao katika ngazi ya juu serikalini na hawafai kumpuuza na kumwalika Dkt Ruto eneo hilo walivyokuwa wakifanya hapo awali.

Naibu Rais amekuwa akijaribu kujinadi kwa wapiga kura katika eneo hilo. Hii ni baada ya ushawishi wake kudidimia kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 ambapo watu wa jamii wa Abagusii walifurushwa kutoka maeneo ya Rift Valley- ambako walikuwa wamenunua mashamba.

Baadhi ya wafuasi wa Naibu Rais wanasema ataendelea kujitafutia umaarufu katika eneo la Gusii licha ya kupandishwa hadhi ya Dkt Matiang’i .

Hata hivyo, wengine wamebadili mkondo na sasa huandamana na Waziri huyo anapohudhuria hafla mbalimbali eneo hilo. Na wengine hupiga kambi katika jumba la Harambee kusaka nafasi ya kushauriana na Dkt Matiang’i.

Kabla ya Dkt Matiang’i kupandishwa cheo serikalini, wanasiasa wa eneo hilo walikuwa wakishindana kumwalika Dkt Ruto katika maeneo bunge yao.

Na katika kipindi cha mwezi mmoja, naibu rais alikuwa amefanya ziara katika maeneo bunge manane kati ya 13 eneo hilo.

Baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo alizindua katika eneo hilo mwaka jana imekwama au inatekelezwa taratibu.

Sasa wabunge wa eneo hilo watalazimika kusaka usaidizi kutoka kwa Dkt Matiang’i ili kukwamua miradi hiyo.

Dkt Andrew Mokaya Maubi, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, anasema mamlaka sasa yako mikononi mwa Dkt Matiang’i na sharti wanasiasa kutoka Gusii wafanye kazi naye.

Kabla ya kuteuliwa kwa Dkt Matiang’i, anasema Dkt Maubi, Ruto alizindua miradi mingi katika maeneo ya Nyanza, Magharibi, Pwani na Mashariki.

“Tunatarajia kwamba viongozi wetu wanapigania kuanzishwa kwa maendeleo katika maeneo yao kwani huu ndio wajibu wao mkuu,” alisema mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Kenyatta anayetoka eneobunge la Kitutu Chache Kusini, Kaunti ya Kisii.

Mbunge wa Mugirango Magharibi, Bw Vincent Kemosi, ambaye ingawa sio mwandani wa Ruto, anasema kupandishwa hadhi kwa Dkt Matiang’i hakutazima nyota ya naibu huyo wa rais katika eneo hilo.

“Wenzangu ambao humuunga mkono wako huru kufanya hivyo, kwani hiyo ni haki yao ya kidemokrasia,” akasema.

Bw Kemosi alifafanua kuwa Dkt Matiang’i ni afisa wa serikali na wanasiasa hawafai kujihusisha naye kisiasa.

You can share this post!

Waliofungwa maisha kwa kumficha gaidi wa Al Qaeda waomba...

WASONGA: Tamko la Ruto ni hatari katika vita dhidi ya...

adminleo