• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Uhuru awaka Rotich akisukumwa kwa kona

Uhuru awaka Rotich akisukumwa kwa kona

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne aliwanyeshea cheche za moto wandani wa Naibu Rais William Ruto kwa kumuita ‘mwizi mkuu’, na akawaambia wana uhuru wa kumripoti kwa idara husika badala ya kumshambulia mazishini.

“Niliona mwingine akisema sijui nimeiba mali ya nani… mimi namwambia aende katika makao makuu ya DCI katika barabara ya Kiambu aseme kile Uhuru ameiba, shida iko wapi? Nitajitetea!” alisema Rais Kenyatta ambaye alionekana mwenye hasira nyingi.

Mnamo Jumapili, wabunge wa mrengo wa Dkt Ruto wakiongozwa na Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, walimshutumu Rais Kenyatta kwa madai ya kutumia vita dhidi ya ufisadi kumhujumu naibu wake.

“Wakati Ruto aliunga Raila mkono 2007 hakuwa mwizi, wakati Ruto aliunga Uhuru 2013 hakuwa mwizi. Saa hii wakati wake wa kuwa rais umefika ndio mnambandika jina mwizi? Tunawajua nyinyi ndio wezi wakuu, na wakati umefika mfahamu kuwa Ruto ana watu wa kumtetea,” alisema Bw Sudi.

Naye Mbunge wa Kimilili, Didmus Barasa alimshutumu Rais Kenyatta akimtaja kama “fisi anayewala wanawe kwa kutumia vijisababu vya ufisadi.”

Akiongea wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Sita kuhusu Ugatuzi katika Kaunti ya Kirinyaga jana, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa vita dhidi ya ufisadi havilengi mtu au jamii fulani.

Alisema juhudi za kupambana na ufisadi hazitafaulu iwapo viongozi wataendelea kujitetea katika hafla za mazishi kuhusiana na kashfa za ufisadi, badala ya kushirikiana na taasisi za uchunguzi.

Jana, bila kuwataja jina wandani wa Dkt Ruto moja kwa moja, Rais Kenyatta aliwashambulia viongozi wanaopinga vita vya ufisadi akisema hatayumbishwa na vitisho vya watu ‘wanaopayuka’ kila mara: “Kupiga kelele katika mazishi hakutasaidia au kuokoa yeyote, sharti tuue zimwi la ufisadi.”

Rais alisisitiza imani yake kwa taasisi za kukabiliana na ufisadi, ambazo ni Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Mamlaka ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Mashtaka ya Umma (DPP).

“Mimi na Wakenya wengi tuna imani na taasisi zinazopambana na ufisadi na tutaendelea kuziunga mkono hadi mwisho,” akasema Rais.

Wiki iliyopita, Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Kipchumba Murkomen alimshutumu Mkurugenzi wa DCI, George Kinoti kwa madai ya kutumiwa na watu fulani kuzima ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.

Dkt Ruto mwenyewe ametaja uchunguzi wa Sh21 bilioni katika sakata ya mradi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet kuwa ‘uwongo mtupu’

Rais aliwaka huku waziri wake wa fedha, Henry Rotich akihojiwa kwa zaidi ya saa 10 katika makao makuu ya DCI, kuhusiana na sakata ya mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Bw Rotich aliwasili katika makao hayo mwendo wa saa kumi na moja alfajiri alikotolewa kijacho mchana kutwa kuhusiana na sakata hiyo ya Sh21 bilioni.

Duru katika DCI zilidokea Taifa Leo kuwa waziri huyo alikabiliwa na wakati mgumu kujibu zaidi ya maswali 300 kuhusu jinsi kampuni ya moja ya Italia ilivyolipwa mabilioni ya pesa, hata kabla ya kuanza kazi ya kuchimba mabwawa hayo.

Bw Rotich pia alitakikana kueleza kwa nini alipuuza ushauri wa Mkuu wa Sheria wa kutoipatia kandarasi kampuni hiyo ya Italia kwa sababu ilikuwa imefilisika.

Iwapo atapatikana na hatia, Bw Rotich huenda akashtakiwa kwa tuhuma za ufisadi.

You can share this post!

Aibu msafishaji kuiba kompyuta ya NMG

Wauguzi sasa kuajiriwa kwa kandarasi

adminleo