• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Madiwani wataka fedha zao zisipitie kwa serikali za kaunti

Madiwani wataka fedha zao zisipitie kwa serikali za kaunti

Na GRACE GITAU

MADIWANI sasa wanataka wawe wakipewa fedha za kutumia katika mabunge ya kaunti moja kwa moja kutoka kwa Serikali Kuu, bila kupitia serikali za Kaunti.

Wakizungumza katika kongamano la Sita la Ugatuzi, mwenyekiti wa mabunge ya kaunti, Bw Johnson Osoi, aliwataka maseneta kubuni sheria itakayowawezesha madiwani kujifanyia maamuzi jinsi ya kutumia fedha, bila kupitia kwa serikali ya kaunti.

Madiwani pia waliwataka maseneta kutunga sheria itakayotambua muungano wa mabunge ya kaunti zote 47.

Mabunge ya kaunti yamekuwa yakishinikiza kupewa fedha zao moja kwa moja kutoka kwa serikali ya kitaifa tofauti na sasa ambapo fedha zao zinapitia kwa serikali za kaunti.

“Mabunge ya kaunti sasa yanategemea fedha kutoka serikali za kaunti. Hali hii imesababisha kutatizika kwa shughuli za mabunge ya kaunti. Suala hili linafaa kuchukuliwa kwa uzito,” akasema Bw Osoi.

Mabunge ya kaunti hayaruhusiwi kupata fedha kupitia mfumo wa kusimamia fedha wa IFMIS.

Magavana wanahofia kuwa huenda mabunge ya kaunti yakafuja fedha iwapo yataruhusiwa kupokea hela hizo katika mfumo wa IFMIS.

Bw Osoi alisema kuwa madiwani wataunga mkono hoja ya kutaka kufanyika kwa kura ya maamuzi iwapo tu hatua hiyo itasaidia kuboresha ugatuzi.

“Tuko tayari kuunga mkono wito wa kura ya maamuzi lakini ni sharti mabadiliko hayo ya katiba yalenge kuboresha ugatuzi. Wakenya tayari wameanza kuvuna matunda ya ugatuzi na sasa tunafaa kuuboresha zaidi,” akasema.

Kiongozi wa Wachache katika Seneti, Bw James Orengo aliwahakikishia madiwani kuwa maseneta wanaendelea kutathmini mswada kuhusu hazina ya ustawishaji wa wadi.

“Mswada huo unaofadhiliwa na Seneta wa Murang’a, Irungu Kang’ata uko katika seneti na nadhani utakuwa wa manufaa makubwa kwani unalenga kuhakikisha kuwa fedha zinapelekwa katika wadi,” akasema Bw Orengo.

Mswada huo unalenga kuhakikisha kuwa kila wadi inatengewa fedha za kuendesha miradi ya maendeleo.

You can share this post!

Mfanyabiashara adai Biwott alikufa na deni lake la Sh6.7...

Watoto 282 waliofanya KCPE Laikipia hawajulikani waliko

adminleo