• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
Jeshi latwaa uwanja wa ndege Nairobi

Jeshi latwaa uwanja wa ndege Nairobi

Na VALENTINE OBARA

JESHI la Taifa (KDF) lilichukua usimamizi wa usalama katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) baada ya wafanyakazi kugoma Jumatno.

Serikali ilisema maafisa wa jeshi la wanahewa watasimamia shughuli za kukagua wasafiri wanaoingia na kutoka katika uwanja huo, pamoja na mizigo yao hadi hali ya kawaida itakaporejelewa.

Chama cha Wafanyakazi wa Ndege (KAWU) kilianzisha mgomo ambao ulitatiza shughuli kuanzia saa kumi na mbili alfajiri, huku hofu ya kiusalama ikitokea.

Mgomo huo pia uliathiri shughuli katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Moi mjini Mombasa na ule wa Kisumu pamoja na Eldoret.

Ndege ya kwanza ilifanikiwa kuondoka JKIA saa sita na robo adhuhuri, huku mashirika ya ndege yakilazimika kufutilia mbali safari zao, hali iliyofanya mamia ya wasafiri kukwama.

Maafisa wa GSU walitumia nguvu asubuhi kutawanya wanachama wa KAWU, ambao walikuwa wanalalamikia usimamizi mbaya wa Mamlaka ya Ndege ya Kenya (KAA) na Shirika la Ndege la Kitaifa la Kenya Airways (KQ).

Ingawa Waziri wa Uchukuzi, Bw James Macharia alikuwa ameahidi ndege ya kwanza ingeondoka saa nne unusu asubuhi kisha shughuli za kawaida zirejelewe, wasimamizi wa KAA na KQ walitofautiana naye.

Mkurugenzi Mkuu wa KAA, Bw Jonny Andersen, alitoa msimamo tofauti na waziri akieleza ingekuwa vigumu hali kurejea kuwa ya kawaida kwa haraka.

“Ifikapo kesho ndipo tutaweza kurudia hali ya kawaida kwa asilimia 100. Unapopoteza saa sita katika kituo kikuu kama JKIA, ni lazima kutakuwa na athari kubwa. Ndege moja ikichelewa inaathiri zinazofuata. Shughuli zitarudi kawaida, lakini itachukua muda,” akasema.

Mkurugenzi Mkuu wa KQ, Bw Sebastian Mikosz naye alisema ndege 24 za shirika hilo zilichelewa, huku mbili zikilazimika kutua katika viwanja vingine vya ndege.

Kwenye purukushani zilizotokea wakati GSU walipokuwa wakitawanya waandamanaji uwanja wa ndege, ilidaiwa kuna watu waliojeruhiwa huku Katibu Mkuu wa KAWU, Bw Moses Ndiema akikamatwa.

Bw Macharia alitetea polisi kwa kutumia nguvu kutawanya waandamanaji hao: “Tulilazimika kutumia nguvu kuwaondoa wahalifu hao hapa. Kama umegoma, kaa nyumbani usije hapa kutatiza shughuli.”

Hayo yalitokea wakati ambapo kuna mzozo kuhusu mpango wa KQ kuchukua usimamizi wa JKIA, hatua ambayo imepingwa vikali na baadhi ya viongozi na wananchi, ikizingatiwa jinsi KQ imekuwa ikipata hasara kubwa kwa miaka kadhaa sasa.

You can share this post!

Baba kizimbani kwa kufanya ngono na bintiye

Afurushwa nyumbani kwa kuzaa na babake mzazi

adminleo