• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Gor Mahia yatulia Misri ikisubiri marudiano na Zamalek

Gor Mahia yatulia Misri ikisubiri marudiano na Zamalek

Na CECIL ODONGO

MABINGWA mara 17 wa Ligi Kuu ya Kenya Gor Mahia wanaendelea na mazoezi kabambe nchini Misri wanakokita kambi kabla ya mtanange wa kufa mtu dhidi ya Zamalek FC siku ya Jumapili.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo akiwa Cairo, Afisa Mkuu Mtendaji wa K’Ogalo Ludorvic Aduda amesema kwamba kikosi kina mori na wanalenga kuwaliza wenyeji ili kurejea katika nafasi ya kwanza kwenye kundi D la Kombe la Mashirikisho Barani Afrika(CAF).

Gor Mahia waliwashinda Zamalek FC 4-2 katika mkondo wa kwanza uliogaragazwa uga wa MISC, Kasarani.

“Kila kitu kiko shwari tangu tutue hapa kutoka Algeria siku ya Jumatatu. Tulipata mapokezi mazuri na kikosi kinaendelea na mazoezi makali kikilenga kuwalaza wenyeji na kuimarisha nafasi yetu ya kufuzu hatua ya robo fainali.

“Kinyume na Algiers tulikoonyeshwa kila aina ya ufidhuli, ubalozi wa Kenya hapa Cairo umefanya kila juhudi kuhakikisha hakuna tunachokikosa. Tunalala vizuri na hatuna ya kulalamikia tunaposuburi kujibwaga uwanjani siku ya Jumapili,” akasema Aduda.

Akigusia utata uliozingira mechi yao dhidi ya NA Hussein Dey ambako walinyimwa bao la wazi, Aduda alishukuru Shirikisho la Soka nchini(FKF) kwa kuwasilisha malalamishi yao kwa Shirikisho la Soka Barani (CAF) lakini akasisitiza kuwa lengo lao kuu kwa sasa ni kujitahidi kushinda mechi mbili zinazosalia.

“Baada ya Zamalek tutakuwa nyumbani dhidi ya Petro de Luanda ya Angola. Ingawa mechi iliyopita ilikuwa na utata na hata tukanyimwa bao la wazi, tumeachia FKF kushughulikia suala hilo kisheria tukisubiri uamuzi baadaye. Hata hivyo sasa tunaangazia sana mechi zijazo na uwezo wetu wa kufuzu,” akaongeza afisa huyo.

Hata hivyo imebainika vijana wa K’Ogalo watakosa huduma za mshambulizi Dennis Oliech anayeuguza jeraha na beki wao raia wa Uganda Shafiq Batambuze kutokana na kupokezwa kadi mbili za manjano kwenye mechi za awali.

You can share this post!

Kicheko mshukiwa kutetemeka huku jasho la kizimbani...

KIBARUA EUROPA: Arsenal na Chelsea wahangaikia Uropa

adminleo