• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
KIBARUA EUROPA: Arsenal na Chelsea wahangaikia Uropa

KIBARUA EUROPA: Arsenal na Chelsea wahangaikia Uropa

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

KOCHA Unai Emery leo Alhamisi usiku ataongoza vijana wake wa Arsenal ugenini dhidi ya Rennes ya Ufaransa katika pambano la Europa League la mkondo wa kwanza unaojumuisha timu 16 bora.

Emery ambaye anajivunia ujuzi wa miaka mingi kwenye mashindano hayo, aliiongoza Seville ya Uhispania kutwaa ubingwa wa taji hilo mara tatu mfululizo.

Akizungumza kabla ya kukutana na BATE Borisov katika raundi ya 32 bora, Emery alieleza malengo yake ya kurejea kwa kishindo katika soka ya bara msimu huu wa 2019/2020 akiwa na Arsenal.

Mesut Ozil. Picha/ Maktaba

“Mawazo yangu ni kwamba kila mechi ni mtihani mkubwa,” aliwaambia waandishi.

“Kwa mfano, nchini Uingereza, taji la EPL, Carabao Cup, FA Cup na hata hili la Europa League, zote ni muhimu. Lengo letu ni kucheza katika michuano ya Klabu Bingwa msimu ujao.”

“Sio rahisi kufuzu kwa mechi hizo, lakini tutajaribu tuwezavyo. Baada ya kuagana na BATE katika hatua ya 32 bora, tungali na kibarua kingine kwenye kampeni zetu,” alisema kocha Emery.

“Tutahitaji kujitahidi vilivyo, tujiamini ili tufaulu katika malengo yetu.

Matumaini makubwa

Kama ilivyotajwa hapo awali, mashindano haya sio mageni kwa Emery ambaye ujuzi wake wa miaka mingi unawapa mashabiki wa Arsenal matumaini makubwa.

Msimu wa 2009/2010, alikuwa na Valencia ambayo ilipangiwa katika kundi moja na Lille Slavia, Prague na Genoa katika hatua ya 32 bora.

Valencia ilitinga hatua ya 16 ambapo iliibwaga Club Brugge ya Ubelgiji na kupangiwa na Bremen ambapo matokeo ya mkondo wa kwanza yalikuwa 1-1 kabla ya timu hizo kufungana 4-4 katika mechi ya marudiano kabla ya kubanduliwa nje na Atletico Madrid ya Uhispania.

Msimu wa 2011/2012 aliiwezesha Valencia kumaliza katika nafasi ya tatu katika mechi za makundi za Klabu Bingwa na kushushwa hadi Europa League ambapo ilipangiwa kucheza na Stoke City kwenye hatua ya 32 bora ambapo vijana wake walishinda kwa 1-0 katika mikondo yote miwili.

Njiani, waliinyoa PSV Eidhoven ya Uholanzi kwa jumla ya ushindi wa 5-3 kabla ya baadaye kuondolewa tena na Atletico Madrid.

Chelsea mwenyeji wa Dynamo Kyiv

Kwingineko, Chelsea inatarajiwa kutumia kiwango chao bora cha sasa kuendea ushindi watakapokabiliana na Dynamo Kyiv katika pambano la mkondo wa kwanza la 16-bora ugani Stamford Bridge jijini London.

Kabla ya ushindi wao mfululizo dhidi ya Tottenham Hotspur na Fulham, kocha Maurizio Sarri alikabiliwa na presha ya mashabiki kufuatia kichapo cha 6-0 kutoka kwa Manchester City na baadaye kubaduliwa nje tena katika fainali ya FA Cup.

Ushindi wao mfululizo umewarejesha katika nafasi nzuri ya kumaliza miongoni mwa nne bora ikikumbukwa kwamba wamecheza mechi chache ligini kuliko Manchester United na Arsenal.

Chelsea walimaliza mechi za makundi katika nafasi ya kwanza baada ya kuitandika Malmo ya Sweden kwa jumla ya mabao 5-1.

Ratiba ya mechi za leo kwa ufupi ni: Eintacht na Inter Milan; Sevilla na Slavia Praha; Zenit na Villarreal; Rennes na Arsenal; Dinamo Zagreb na Benfica; Valencia na FC Krasnodar; Napoli na Red Bull; Chelsea na Dynamo Kyiv.

You can share this post!

Gor Mahia yatulia Misri ikisubiri marudiano na Zamalek

Mabingwa watetezi UEFA wasalimu amri

adminleo