• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wanawake nyota waliong’aa katika fani mbalimbali

Wanawake nyota waliong’aa katika fani mbalimbali

NA LEONARD ONYANGO

Huku ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Machi 8, 2019, Taifa Leo Dijitali inaangazia wanawake sita wa humu nchini ambao wametambuliwa kwa juhudi zao kuifaa jamii.

Koki Mutungi – RUBANI

Alikuwa rubani wa kwanza wa kike wa Kenya Airways mnamo 1993. Mnamo 2014, aliandikisha historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kutunukiwa cheti cha kuendesha ndege ya Boeing 787 ‘Dreamliner.’

Bi Mutungi (pichani juu) alizaliwa 1979 na alisomea urubani katika Chuo cha Marubani kilichoko katika uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi. Alijiendeleza kimasomo katika Chuo cha marubani cha Oklahoma, Amerika.

Mnamo 2014, Bi Mutungi aliongoza kikosi cha marubani wa kike wa Kenya Airways walioleta ndege ya nne aina ya B787-8 Dreamliner nchini Kenya kutoka Amerika.

Marjorie Oludhe MacGoye – MWANDISHI

Ni miongoni mwa waandishi wa vitabu waliotia fora barani Afrika kutokana na weledi wake katika uandishi wa riwaya, hadithi fupi, mashairi na hadithi za watoto.

Bi MacGoye alizaliwa 1928 jijini Southampton, Uingereza na aliwasili Nairobi mnamo 1954 akiwa mmishenari wa kuuza vitabu. Miaka sita baadaye, alifunga ndoa na Daniel Oludhe MacGoye aliyekuwa daktari.

Baada ya fungate 1960, Bi Macgoye aliacha kazi yake ya kuuza vitabu akahamia Kisumu na kutangamana na jamii ya Waluo.

Kitabu chake cha kwanza kilikuwa: Victoria and Murder in Majengo kilichochapishwa 1972. Vitabu vyake vingine ni Street Life, The Present Moment, Chira, Coming to Birth, A farm Called Kishinev. Kitabu chake cha mashairi kilichofana ni Song of Nyarloka and other Poems.

Vitabu vya MacGoye vilishinda tuzo tele humu nchini na kimataifa.

Aliaga dunia mnamo Desemba 1, 2015.

Profesa Olive Mugenda- USIMAMIZI/ELIMU

Prof Mugenda ndiye mwanamke wa kwanza nchini kuwa Naibu Chansela wa Chuo cha Umma.

“Nilizaliwa katika eneo la Kikuyu. Wazazi wangu waliachana tukiwa wadogo hivyo mamangu akajitwika jukumu la kutulea,” asema Prof Mugenda.

“Tulikuwa watoto wanne na mama alilazimika kutulea kwa kutumia mshahara wa ualimu,” anaongezea.

Prof Mugenda alisomea katika Shule ya Upili ya Alliance ambapo alifanya vyema na kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta. Alipata daraja la kwanza na kupata ufadhili wa kusomea Elimu kiwango cha uzamili katika Chuo Kikuu cha Iowa, Amerika.

Baada ya kuhitimu masomo yake ya uzamili, alipata ufadhili wa kusomea masuala ya familia, elimu na utafiti kiwango cha uzamifu (PhD).

Baada ya kuhitimu PhD, alirejea nchini Kenya na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Alipanda daraja na kufikia 2006, aliteuliwa Naibu wa Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta baada ya kuwabwaga washindani wake watatu wa kiume katika mahojiano.

Prof Mugenda alikuwa Naibu Chansela wa kwanza wa chuo kikuu cha umma, lakini mwanamke wa pili kuongoza chuo kikuu nchini Kenya baada ya Prof Leah Marangu aliyeongoza chuo cha kibinafsi cha African Nazarene.

Prof Mugenda alifana katika kuboresha miundomsingi na kiwango cha masomo alipokuwa Naibu Chansela wa Chuo cha Kenyatta kwa miaka 10.

Miongoni mwa miundomsingi hiyo ni ujenzi wa hospitali kubwa ya rufaa na mafunzo.

Prof Mugenda alistaafu kutoka wadhifa wa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta mnamo 2016.

Aliapishwa kuwa mjumbe wa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) Novemba 2018.

Tabitha Karanja – BIASHARA

Ni mwasisi na Mkurugenzi Mkuu wa Keroche Breweries ambayo imetoa ushindani mkali kwa kampuni za kimataifa za kutengeneza mvinyo.

Mnamo 2014, alitajwa na jarida la Forbes kuwa mwanamke aliyetia fora zaidi katika biashara.

Kiwanda cha Keroche kimetoa nafasi za ajira kwa mamia ya Wakenya.

Bi Karanja alianza safari ya kutengeneza vileo miaka ya 1990, mumewe, Joseph Karanja, alipofunga duka lake la kuuza vifaa vya ujenzi na kujitosa kat ika biashara ya pombe.

Aliajiri watu 10 waliomsaidia katika biashara hiyo.

“Mume wangu alinishawishi kwamba biashara ya mvinyo ilikuwa nzuri. Nilikubali na nikakumbatia biashara hiyo,” anasema Bi Karanja.

Bi Karanja, hata hivyo, anasema biashara yake ilikumbwa na upinzani si haba.

“Nilishambuliwa na watu kutoka kila upande wakiwemo wanasiasa na maafisa wa serikali ambao waliambia watu kwamba nilikuwa nauza chang’aa. Kuna wakati serikali ilifunga kampuni yangu,” aanasema.

Bi Karanja anasema licha ya mawimbi hayo, alisimama kidete na sasa kampuni ya Keroche Breweries inaendelea kunawiri.

Mnamo 2013, alitunukiwa Tuzo ya Kenya’s Golden kwa kufana katika sekta ya utengenezaji wa kiviwanda. Mnamo 2009, alitunukiwa na Rais Mwai Kibaki tuzo ya Moran of the Burning Spear (MBS).

Mnamo 2016, Bi Karanja alikuwa mwanamke wa kwanza nchini Kenya kutunukiwa Tuzo ya Entrepreneurial Excellence in Africa kwa kufana katika biashara. Wengine ambao wamewahi kutunukiwa tuzo hiyo ni Rais Mstaafu Mwai Kibaki na Dkt Manu Chandaria.

Habari kumhusu Bi Karanja zimechapishwa katika majarida mbalimbali nchini na kimataifa ili kuwatia motisha wengine.

Kampuni ya Keroche inatengeneza vinywaji kama vile Summit Lager na Summit Malt.

Mekatilili wa Menza – UKOMBOZI

Inasadikika kwamba Mekatilili wa Menza alikuwa mwanamke wa kwanza kupigania ukombozi kutoka minyororo ya wakoloni nchini Kenya na katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alipigana na wakoloni katika juhudi za kuhakikisha anahifadhi utamaduni wa jamii ya Wagiriama. Alitumia ulumbi wake kuwashawishi wenyeji kuchukua kiapo na kutoa kafara ambazo zingewasaidia kutwaa mashamba yao yaliyokuwa yametwaliwa na wakoloni.

Kulikuwa na matukio mawili yaliyomchochea Mekatilili wa Menza kukabiliana na wakoloni.

Siku moja Mekatilili pamoja na kaka zake walitembelea eneo la Mtsanganyiko karibu na bahari ya Hindi. Kaka yake mmoja aliyefahamika kwa jina la Mwarandu alitekwa nyara na walanguzi wa watumwa wa Kiarabu na hakuonekana tena.

Jambo jingine lililomchochea ni unabii wa aliyekuwa mganga wa Kigiriama, Mepoho, kwamba watu weupe wenye nywele kama kamba ya katani wangekuja kwa kutumia majahazi na kusababisha mauaji ya watu wa Giriama.

Mekatilili alizaliwa kijijini Mtsara wa Tsatsu kilichoko eneo la Ganze, Kaunti ya Kilifi. Alitoka jamii ya Wamijikenda.

Mekatilili alimhangaisha aliyekuwa Kamishna wa Mkoa wa Pwani Charles Hobley (1912-1919). Mnamo 1913, Hobley aliongoza maaskari wa kikoloni na kwenda kuwalazimisha wazee wawili wa kaya na kuwalazimisha kufichua kiongozi wa ‘waasi’.

Mekatilili na mmoja wa wazee wa Kaya Wanje wa Mwadorikola walikamatwa katika eneo la Sabaki na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano kila mmoja katika gereza la Kisii.

Serikali ya wakoloni pia ilitoza faini jamii ya Wagiriama. Baada ya kushindwa kulipa faini, watu wa jamii ya Wagiriama walilazimishwa kufanya kazi katika mashamba ya wakoloni.

Mekatilili na Wanje walisamehewa na serikali ya wakoloni mnamo 1919.

Serikali ya wakoloni iliteua Wanje kuwa mkuu wa eneo la Kambi na Mekatilili akapewa wadhifa wa mkuu wa Baraza la Wanawake.

Wawili hao walifariki 1920. Mekatilili alifariki akiwa na umri wa miaka 70. Mnamo Desemba 2010, Mekatilili alitambuliwa rasmi kama shujaa na serikali ya Kenya na sanamu yake ikajengwa katika Bustani ya Uhuru Park, Nairobi.

Margaret Wambui Kenyatta

Alikuwa binti wa pekee na mmoja wa watoto wawili wa rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta na mke wake wa kwanza, Grace Wahu.

Alikuwa meya wa kwanza wa kike humu nchini mnamo 1970. Alikuwa balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa (UN) kwa kipindi cha miaka 10.

Alizaliwa 1928 na kusomea katika shule ya msingi ya Ruthimitu. Baadaye alijiunga na Shule ya Upili ya Alliance. Margaret pamoja na nduguye Peter Muigai walilelewa katika mtaa wa Dagoretti, Nairobi.

Alifariki Aprili 5, 2017 akiwa na umri wa miaka 89.

Makala haya yamechapishwa kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board, http://kenyayearbook.co.ke/

You can share this post!

Mahakama haitakuokoa, ODM yamwambia Jumwa

TAHARIRI: Ni wazi hatua za ugatuzi bado hafifu

adminleo