• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
MWANAMKE MWELEDI: ‘Najionea fahari kuilinda nchi’

MWANAMKE MWELEDI: ‘Najionea fahari kuilinda nchi’

Na KENYA YEARBOOK

ALIKUWA mwanamke wa kwanza kuhudumu kama daktari katika hospitali ya kijeshi ya Gilgil Military Garrison Regional Hospital.

Kando na hayo, Meja (Dkt) Stella Mwangi, ni daktari wa kwanza kufanya upasuaji katika shughuli za kijeshi vitani.

Pia, Jeshi la Kenya lilipovamia Somalia katika huduma ya ‘Operation Linda Nchi’, Meja Mwangi alikuwa mstari wa mbele kuratibu shughuli kuhusu afya ya wanajeshi vitani, zilizohusisha hasa kuwarejesha nyumbani waliokuwa na majeraha, vilevile kutoa chanjo.

Isitoshe, pamoja na wafanyakazi wengine katika idara yake, Bi Mwangi ametia bidii kurahisisha shughuli za kuchunguza maradhi ya kansa ya njia ya uzazi bila malipo miongoni mwa wanawake wanaohudumu katika jeshi.

Kwa sasa Meja Mwangi anahudumu katika idara inayoratibu mipango kuhusu virusi vya HIV katika jeshi.

Idara hii inahusika pia na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa kiafya jeshini, vilevile kushirikiana na huduma za afya za vikosi vya jeshi kutoka nchi zingine.

Mzawa wa jiji la Nairobi, familia yake ilichochea ufanisi wake kwa kumhimiza kutia bidii shuleni na kuwa na ndoto kuu maishani.

Meja (Dkt) Stella Mwangi. Picha/ Hisani

Azma yake ya kutaka kuhudumia umma ilianza akiwa mdogo, wakati huo wakiishi mtaani Dagoretti ambapo aliguswa na matatizo yaliyowazonga wakazi.

Ni suala lililomsukuma kufanya kazi kama mhudumu wa kujitolea katika makao ya watoto na wadi za watoto wanaogua kansa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta akiwa likizoni.

Baada ya kufanya vyema katika mtihani wa kitaifa wa KCSE alichagua kusomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo mara alipohitimu alipata agizo la kuhudumu katika hospitali ya Wilaya ya Kitale, alikofanya kazi hadi alipojiunga na jeshi.

Uchu

Mwanzoni suala la kujiunga na jeshi halikuwa mawazoni mwake. Uchu wa kutaka kujiunga na jeshi ulimjia baada ya rafiki yake ambaye pia alikuwa mwanajeshi kumsimulia hadithi za aliyoshuhudia akiwa kikosini.

“Alikuwa ametoka ziarani maeneo ya Lodwar na Isiolo. Hadithi zake hasa zilikuwa kuhusu mandhari tofauti aliyokumbana nayo alipokuwa akihudumu katika kambi na vitani, suala lililonisisimua,” aeleza Meja Mwangi.

Aidha alimueleza kuwa wakati mwingine wanajeshi huitwa kusaidia katika majanga ya kitaifa na hilo likampa motisha zaidi.

Ni hapa alikata kauli kujiunga na jeshi, ambapo baada ya miezi minne ya mafunzo magumu kama kadeti, alihitimu.

Baadaye, alipata agizo la kwenda kuhudumu katika hospitali ya Gilgil Garrison, kisha kupelekwa katika hospitali ya kijeshi ya Forces Memorial Hospital, Januari 2011 ambapo anahudumu kama daktari.

Licha ya kutamba kitaaluma na huduma yake katika jeshi, Meja Mwangi hajaruhusu shughuli hizi zihitilafiane na maisha yake ya kawaida kama mke na mama.

“Mimi ni meja na daktari nikiwa afisini, lakini nikiwa nyumbani mimi ni mama na mke ambapo nawashughulikia mume na binti yangu vilivyo,” aeleza.

Hata hivyo, usipumbazwe na kudhani safari hii imekuwa mteremko.

Kuna wakati amejikuta matatani majukumu yake kama mwanajeshi, mama na mke yanapogongana.

“Kwa mfano wakati wa shughuli ya ‘Operation Linda Nchi’ nililazimika kusafiri ghafla. Hata hivyo, mume wangu alinisaidia sana kwani alihakikisha kwamba binti yetu anastahimili maisha bila mimi. Pia nikiwa nchini Somalia, nilijaribu kupiga simu angaa mara mbili kwa siku ili kuwasiliana na familia yangu,” aeleza.

Bi Mwangi anashauri kwamba ni muhimu kusawazisha mambo yote maishani mwako.

“Huwezi makinika na kazi pekee na upuuze familia yako. Tunapaswa kuwa waangalifu tusipuuze majukumu tuliyopewa na Mungu ya kuwa wake na akina mama,” aeleza.

Zaidi ya yote anasema kwamba imani yake imekuwa msingi wa ufanisi wake.

“Kama Mkristu nimejifunza kwamba maombi ni muhimu sana katika maisha ya kila siku. Kwa hivyo kila Jumapili nachukua fursa hiyo kuhudhuria ibada kanisani,” asema.

Kwa sasa azma yake ni kuendeleza taaluma yake zaidi hasa katika sekta ya afya ya umma na matatizo ya kiakili.

“Pia ningependa kuimarisha sera za kiafya katika kikosi cha jeshi ili kuhakikisha kwamba wanajeshi wako thabiti kiakili, na hivyo wako tayari kuhudumu,” aongeza.

Pia, anasema kwamba ni ndoto yake kuona muundomsingi ya kimatibabu hasa katika kikosi cha jeshi na Wakenya wote kwa jumla, inaimarishwa.

Zaidi ya yote anawarai wanawake zaidi kujiunga na jeshi.

“Baadhi ya wanawake huogopa kujiunga na jeshi kutokana na fikra kwamba mafunzo yanayohitajika ni magumu na ya kuchosha, lakini ningependa kuwaambia wasiogope,” asema, huku akiongeza kwamba mbali na masharti bora ya uajiri, kuna fursa nyingi kwa wanawake wenye taaluma.

You can share this post!

Siku ya Wanawake yaletea tabasamu wafungwa wanawake Thika

SHANGAZI AKUJIBU: Nilimfumania peupe na sasa ataka nimsamehe

adminleo