• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
DAU LA MAISHA: Mwanamazingira mwenye ndoto kuu

DAU LA MAISHA: Mwanamazingira mwenye ndoto kuu

Na PAULINE ONGAJI

HUKU Kenya ikiendelea kupambana na suala la uharibifu wa misitu, amejitwika jukumu la kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti.

Katika umri wa miaka 19 pekee, Lily Tanui anatoa mfano mwema kwa vijana na kufikia sasa, ameongoza shughuli ya upanzi wa zaidi ya miti 5,000 katika sehemu mbalimbali.

Ni juhudi ambazo ameendeleza kupitia shirika la Tree Growers Association of Kenya aliloanzisha mwaka 2018, ambapo baadhi ya maeneo yaliyonufaika ni mjini Eldoret, nyumbani kwao eneo la Eldama Ravine, katika shule yake ya zamani ya Bunyore Girls na misitu tofauti.

Bi Lily Tanui mwanaharakati wa Uhifadhi wa Mazingira na mwanzilishi wa shirika la uhifadhi la Tree Growers Association of Kenya katika jumba la Nation Machi 6, 2019. Picha/ Kanyiri Wahito

“Pia nimeongoza upanzi wa miti katika shule na makanisa mbalimbali, misitu kama vile Ngong, Kaptagat, na Kibiku,” aeleza Bi Tanui.

Ameafikia haya kwa kuhusisha jamii kupitia kampeni za uhamasishaji kuhusu umuhimu wa kupanda miti na kushughulikia mazingira kwa kuandaa mikutano na katika mitandao ya kijamii.

Na kama wasemavyo wahenga kwamba chanda chema huvikwa pete, Bi Tanui anazidi kutambuliwa kutokana na jitihada zake.

Kwa mfano ameteuliwa katika tuzo za Diara Awards Environmental and Conservation Champion Awards, tuzo zinazowatambua watu wanaojizatiti kuhifadhi mazingira huku mshindi akitarajiwa kutangazwa Aprili.

Isitoshe, mwaka wa 2016, alipata mwaliko wa kuhudhuria hafla ya masuala ya nishati na mazingira ya Yale Young Global Scholars nchini Amerika ambapo alijifunza kuhusu nishati ya maumbile asilia kama vile jua, upepo na mawimbi.

Pia juhudi zake zimemwezesha kupata mialiko ya kuhudhuria warsha mbalimbali za kimazingira.

“Nimebahatika kuhudhuria warsha mbalimbali za kimazingira kama vile United Nations Environment Assembly, Global Landscapes Forum, Workshop for Environmental Human Rights Defenders na Clear the Air Conference,” aleleza.

Safari yake ilianza akiwa na miaka 12 pekee alipoanza kuvutiwa na ulimwengu wa viumbe huku azma yake ikichochewa na marehemu Prof Wangari Maathai.

Aunda chama cha mazingira

Ni suala lililomsukuma zaidi hata alipojiunga na shule ya Bunyore Girls’ High School ambapo alikuwa mwanafunzi wa kwanza kuunda chama cha mazingira na hata kuongoza upanzi wa zaidi ya miti 2,000.

Aidha alitoa mafunzo kuhusu mazingira shuleni, suala lililomfanya kuteuliwa kama kiranja wa mazingira mwaka wa 2016 wakati huo akiwa katika kidato cha tatu,” aeleza.

Penzi lake kuu katika masuala ya mazingira lilichochewa na babake ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mitishamba.

“Babangu, Dkt Shadrack Moimett ni daktari wa mitishamba na nilipokuwa naendelea kukomaa niligundua nilivutiwa sana na miti inayotumika kutengeneza dawa, na hii pia ilinisukuma kuwa mwanaharakati wa mazingira,” aeleza.

Baada ya hapa alimhimiza baba yake kuzidi kupanda miti ya kiasili ili kumuepusha na safari ndefu za kwenda kutafuta viungo muhimu kuunda dawa zake.

“Hapa nilihakikisha kwamba katika kipande cha ardhi cha ekari moja nyumbani kwetu tulipanda miti ya kiasili, na hivyo kuanzisha rasmi safari hii,” aeleza.

Kwa sasa Bi Tanui anatumai kusomea masuala ya kimazingira chuoni.

“Pia, ndoto yangu ni kwamba shirika langu la Tree Growers Association of Kenya litafanikiwa kupanda zaidi ya miti milioni kumi ifikapo mwaka wa 2027, katika harakati za kuhamasisha zaidi vijana kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira,” aeleza.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Nilimfumania peupe na sasa ataka nimsamehe

SHERIA: Ndoa muungano wa hiari ila sharti sheria ifuatwe

adminleo