• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Ripoti yaonyesha bado kuna pengo katika usawa wa jinsia

Ripoti yaonyesha bado kuna pengo katika usawa wa jinsia

Na AFP

SIKU ya Wanawake ya Kimataifa ilipoadhimishwa Ijumaa, ripoti ilidokeza kuwa idadi ya wanawake wanaoshughulika na majukumu ya nyumbani ingali juu ikilinganishwa na ile ya wanaume.

Ripoti hiyo ya Shirika la Kimataifa la Leba (ILO), ilisema kuwa idadi ya wanaume wanaofanya kazi zisizokuwa na faida ya malipo nyumbani, kama vile kulea watoto, kuosha vyombo, kusafisha nyumba na kufua nguo, imeongezeka hadi milioni 41.

Wanawake waandamana Machi 8, 2019, kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani eneo la Guadalajara, jimbo la Jalisco, Mexico kama njia ya kushinikiza usawa wa kijinsia. Picha/ AFP

Ripoti hiyo inasema kuwa asilimia 22 ya wanawake wa kati ya umri wa miaka 18 na 50 wanafanya kazi za bure nyumbani kote duniani.

“Katika mataifa ya Uarabuni, asilimia 60 ya wanawake wamekatazwa kutafuta ajira na waume wao na badala yake wanafanya kazi za nyumbani kama vile kulea watoto, kufua, kupika, na kadhalika,” inasema ripoti hiyo.

Wanaume ambao hawajaajiriwa na wanafanya kazi za nyumbani bila malipo ni sawa na asilimia 1.5 pekee.

Ripoti hiyo ya ILO, hata hivyo inasema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wanawake wanaopata ajira katika kipindi cha miaka 27 iliyopita.

Utafiti wa kura ya maoni uliofanywa na ILO mwaka jana, ulibaini kuwa idadi kubwa ya wanawake wanapendelea kuajiriwa badala ya kusalia nyumbani kulea watoto.

“Katika kipindi cha miaka 20, muda ambao wanawake wanatumia kufanya kazi za nyumbani zisizolipwa umepungua. Kwa upande mwingine, idadi ya wanaume ambao sasa wanafanya kazi za nyumbani zisizo na mshahara kama vile kulea watoto, upishi, kusafisha nyumba imeongezeka,” akasema Manuela Tomei, Mkuu wa Idara ya Usawa kazini, ILO.

Alisema kuwa itachukua miaka 200 kuwepo kwa idadi sawa ya wanawake na wanaume wanaofanya kazi zisizo na mshahara nyumbani.

Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa wanawake pia hujitwika jukumu la kufanya kazi bila malipo kama vile kuchemsha chai katika afisi wanakofanyia kazi.

“Wanaume wanafaa kushirikiana na wanawake kufanya kazi za nyumbani. Wanaume wakikumbatia kazi za nyumbani basi kutakuwa na usawa,” inasema ripoti.

Muda

Wanawake wanafanya kazi za nyumbani zisizo na mshahara kwa wastani wa saa nne na dakika 25 kwa siku kote duniani.

Wanaume wanafanya kazi za nyumbani kwa wastani wa saa moja na dakika 23 kwa siku na kutumia muda uliosalia kufanya mambo ya kujiburudisha kama vile kutazama runinga.

“Hata wanawake wanapoajiriwa kwa afisi hufanya kazi zisizo na mshahara. Wanawake wanapumzika kwa muda mfupi na hilo linaathiri afya yao,” inasema.

Ripoti ya ILO inasema kuwa wastani wa mshahara ambao wanawake wanalipwa ni kidogo kwa asilimia 20 ikilinganishwa na wanaume.

“Katika mataifa ya Pakistan na Saudi Arabia pengo la mshahara kati ya wanawake na wanaume ni asilimia 40,” inasema ripoti.

You can share this post!

Ajificha chooni kuhepa mademu

BI TAIFA, JUMAMOSI, MACHI 9, 2019

adminleo