• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Murkomen aitwa DCI kuhusu mabwawa

Murkomen aitwa DCI kuhusu mabwawa

Na BENSON MATHEKA

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji sasa anamtaka Seneta wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen, kufika makao makuu ya Mkurugenzi wa Ujasusi (DCI) kutoa taarifa kuhusiana na sakata ya mabwawa ya Arror na Kimwerer yaliyo katika kaunti yake.

Hii ni baada ya Bw Murkomen kukosoa taarifa ya Bw Haji kuhusu sakata hiyo akisema ilikuwa na makosa makubwa mno na kuashiria kwamba yalitokana na ukosefu wa kufahamu mfumo uliotumiwa kutoa malipo kwa kampuni inayojenga mabwawa ya Arror na Kimwerer.

Afisi ya DPP, kupitia akaunti yake ya Twitter ilimtaka Bw Murkomen kuwasilisha anayofahamu kwa wapelelezi.

Akijibu taarifa ambayo Bw Haji alitoa Ijumaa jioni, Bw Murkomen alijitolea kumfunza DPP na DCI jinsi malipo ya zabuni yanayofanywa akisema yeye ni mmoja wa wataalamu wachache nchini katika sekta hiyo.

“Nimeeleza ninachochukulia kuwa makosa ya kisheria na ukweli kutokana na tajiriba yangu katika masuala ya ufadhili wa miradi na mikopo ya kuitekeleza. Iwapo DPP na DCI watahisi wanafaa kutumia ufahamu wangu katika masuala haya, niko tayari kutoa huduma zangu kwa taifa langu,” Bw Murkomen alisema.

“Ingawa tuna wataalamu wachache katika masuala haya, ni matumaini yangu kwamba DPP atafanya kila kitu kuhakikisha ukweli umejulikana. Kuna makosa makubwa katika taarifa yake,” alieleza.

Kwenye taarifa yake, Bw Haji alisema japo uchunguzi unaendelea, kufikia sasa, anaamini madai yaliyoripotiwa kuhusu ufisadi katika utoaji zabuni na malipo yalikuwa na msingi.

Bw Haji alikubaliana na Bw Kinoti kwamba serikali ilipoteza Sh21 bilioni kati ya Sh65 bilioni zilizopaswa kulipwa kampuni ya Italia kwa ujenzi wa mabwawa hayo mawili.

You can share this post!

Hii handisheki ni ndoto tu – Ruto

Basi la shule lageuzwa matatu jijini

adminleo