• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
KINAYA: Msage kabisa ‘Hustler’ la sivyo akusage kabla ya kura za 2022

KINAYA: Msage kabisa ‘Hustler’ la sivyo akusage kabla ya kura za 2022

NA DOUGLAS MUTUA

NAWATAKIA kila la heri wanaowana kwa meno na kucha kumzuia Dkt Samoei Kipchirchir kurithi Ikulu kutoka ‘Kamau wa Pili’.

Naam, kila la heri kwa maana wasipofanya hesabu zao vizuri, mzaliwa huyo wa Sugoi ajipate akilala Ikulu hata siku mbili, wapo watu watakaolia na kusaga meno!

Wajua, Dkt Kipchirchir si mwanasiasa wa kawaida kama ‘Kamau wa Pili’ na ‘Baba’, wajanja wakuu zaidi katika nchi hii wanaojua kuchanganya siasa na maslahi binafsi.

Dkt Kipchirchir akikutambua kama adui, sijamzoea akirudi nyuma kuzingatia maslahi ya siasa wala biashara, kazi yake kukulima na kukuweka mbali naye kabisa!

Walio salama katika vita hivi vya urithi ni ‘Kamau wa Pili’ na ‘Baba’, hasa ikiwa mwana huyo wa Jaramogi atastaafu siasa na kula matunda ya mapambano aliyoshiriki awali.

Wawili hao wako salama kwa maana mmoja ataelekea Gatundu alikotoka na wa pili moja kwa moja mpaka Bondo.

Hata wasipoondoka jijini, Dkt Kipchirchir anaweza kuwasamehe kwa sababu ya ‘uzee’ wao, aseme kumzaba kofi mzee ni kujiletea laana ya bure.

Tena, kumbuka ‘Kamau wa Pili’ na ‘Baba’ ni wajanja. Wanaweza kumwita kando akishinda vita vya kwenda Ikulu wamsadikishe kwamba yeye sasa ni mmoja wao.

Hatuwezi kusema hivyo kuwahusu wanasiasa wachanga, watu wa mkono hasa wanaotumiwa na ‘Kamau wa Pili’ na ‘Baba’ kumponda Daktari wa Sugoi.

Kitu cha kwanza akishinda ni kuwanyorosha watu hao wa mkono na kuhakikisha hawatawahi kuinua kichwa tena kwenye siasa akiwa mcheza-ngoma mkuu kilingeni.

Tafadhali usiniambie eti mchezo wa siasa hauchezwi hivyo. Unadhani siui? Hapa hatumjadili mwanasiasa wa kawaida, tunamjadili Dkt Kipchirchir na damu yake ya moto.

Badala ya kutafuta muafaka na watesi wake wa sasa akiingia Ikulu, atakuwa mbioni kuwakuza wengine wachanga na kujenga himaya kubwa ya vibaraka watakaomsujudia.

Alianza kujenga himaya hiyo mapema mwaka wa 2017 pale chaguzi za michujo ya vyama zilipokuwa zikiendelea.

Alihakikisha watu waliotaka kumzuia asiingie Ikulu hapo 2022 walitifuliwa vumbi na vijogoo wachanga hivi kwamba mpaka sasa haijulikani iwapo watafufuka kisiasa.

Ikiwa umekuwa ukishangaa kwa nini Dkt Kipchirchir anaungwa mkono na wabunge wengi wa eneo la Mlima Kenya kuliko ‘Kamau wa Pili’, basi jua alipanda na sasa anavuna.

Kumbuka ni mwekezaji hodari aliyeapa kuwekeza mbinguni ili njia yake ya kufika huko, akipitia kituo kiitwacho Ikulu, iwe tambarare na pana.

Hilo limewauma wengi, lakini hawajui wamwambie nini ila kudai amelia chunguni cha umma akakwangura mpaka na ukoko!

Tuulizane kiroho safi: ‘Kamau wa Pili’ anapotwambia eti mali ya umma inatafunwa kishezi, hakiri hadharani kuwa kazi aliyoapia Katiba kutekeleza imemshinda?

Inatosha kweli kwa kamanda mzima kuwanyooshea watu kidole na kusema ‘mwizi! mwizi! mwizi!’? Mbona asifyatue mzinga?

Ikiwa haogopi na ana hakika naibu wake ameiba, mbona asitutolee taarifa, anawe mikono, atuambie amewaacha makachero wampeleleze ‘mtu wangu wa mkono’?

Kila mpenda haki atakwambia vita dhidi ya ufisadi visipoanzia kule ufisadi wenyewe ulikoanzia vitatumiwa kama kitanzi cha kumnyonga mbwa mla mayai.

[email protected]

You can share this post!

Sunni Anjuman wanavyoinua maisha ya Waislamu maskini

DINI: Kujipenda binafsi ni mtihani, mtu anaweza kuwa adui...

adminleo