• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Usalama wa ndege aina ya Boeing 737 Max 8 watiliwa shaka

Usalama wa ndege aina ya Boeing 737 Max 8 watiliwa shaka

Na VALENTINE OBARA

HUKU uchunguzi ukianzishwa kuhusu ajali ya ndege iliyokuwa ikitoka Addis Ababa, Ethiopia kuelekea Nairobi Jumapili, maswali yaliibuka upya kuhusu usalama wa aina hiyo ya ndege ya Boeing 737 MAX 8.

Mwaka 2018, ndege aina hiyo hiyo ilianguka baharini mnamo Oktoba na kusababisha vifo vya watu wote 189 nchini Indonesia, dakika 13 pekee baada ya kupaa angani.

Ingawa kumekuwepo mamia ya ajali za ndege za Boeing tangu miaka ya sabini, ajali hizi mbili zinasababisha wasiwasi kwa kuwa 737 MAX 8 ni kati ya aina mpya zaidi za ndege za Boeing, kwani zilizinduliwa 2016.

Ethiopia ilikuwa imepokea ndege yake Novemba mwaka uliopita kutoka kampuni ya Boeing ya Amerika.

Jana, kampuni hiyo ilisema imejitolea kutoa usaidizi kwa shirika la ndege la Ethiopian Airlines endapo itahitajika kufanya hivyo.

Ndege hiyo huwa na uwezo wa kubeba abiria kati ya 162 na 210. Ina urefu wa futi 129 inchi nane kwenda nyuma, na futi 40 inchi nne kwenda juu. Mbawa zake ni futi 117 inchi 10 kila moja.

Katika ajali iliyotokea Indonesia, ambapo pia ndege ya shirika la Lion ilikuwa jipya, ilisemakana kulikuwa na hitilafu za programu zinazowezesha ndege hiyo kuendeshwa kwa teknolojia za kisasa.

Ripoti zilisema programu hizo zilikuwa zimewekwa kwenye mitambo ya ndege ilhali marubani hawakufahamishwa vyema kuzihusu.

Wakati huo huo, Afisa Mkuu wa Boeing, Dennis Muilenburg alinukuliwa akisema wangechukulia ajali hiyo kwa uzito na kujifunza kutokana nayo ili kuboresha usalama wake.

“Tutajifunza kutokana na ajali hii na kuendelea kuboresha usalama wa ndege zetu. Kila siku mamilioni ya watu hutegemea ndege zetu za kibiashara kusafiri kote ulimwenguni kwa njia salama. Wakati hili halifanyiki sisi huchukulia hali hiyo kwa uzito,” akasema.

You can share this post!

Wakenya wasifu hatua ya korti kuzima amri ya NHIF

Machozi yamtiririka polo akinyenyekea mkewe asimteme

adminleo